Aller au contenu
Tafsir As-Saadi - Swahili · Az-Zumar
Sourate 39

Az-Zumar

Voici une traduction du tafsîr d’as-Saʿdī, telle qu’IslamHouse.com la publie sur saadi.islamenc.com, lue dans les pages de ce site. Le site ne dit ni qui l’a traduite ni quelle édition imprimée elle suit, et n’indique aucune condition pour en reprendre le texte, si bien que le droit de la montrer n’est pas vérifié. Personne ne l’a comparée à un livre imprimé, et aucun savant ne l’a relue. Chaque passage se tient à côté des versets qu’il commente, qui sont le texte coranique de Tanzil, montré tel qu’il y est ; un verset auquel le site ne donne aucun commentaire propre se tient avec le passage qui le précède, et l’index nomme chacun de ces versets. Sabīl n’en a rien écrit ni traduit.

Texte desaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)pris le 2026-10-22

Verset 69

وَأَشْرَقَتِ ٱلْأَرْضُ بِنُورِ رَبِّهَا وَوُضِعَ ٱلْكِتَـٰبُ وَجِا۟ىٓءَ بِٱلنَّبِيِّـۧنَ وَٱلشُّهَدَآءِ وَقُضِىَ بَيْنَهُم بِٱلْحَقِّ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ 69

{69} "Na ardhi itang'ara kwa Nuru ya Mola wake Mlezi." Hili linaonyesha kwamba nuru zilizopo zitatoweka Siku ya Kiyama na kupotelea mbali. Kwa maana Mwenyezi Mungu alijulisha kwamba jua litakunjwa, mwezi utapatwa, nyota zitatawanywa, na watu watakuwa gizani. Kisha ardhi itang'aa kwa nuru ya Mola wake Mlezi atakapodhihiri na kushuka ili kuhukumu baina yao. Siku hiyo Mwenyezi Mungu atawapa nguvu viumbe, na atawaumba kwa namna ya kwamba watakuwa na nguvu ya kutoweza kuunguzwa nuru yake, na pia wataweza kumuona, vinginevyo, nuru yake ni kubwa, kama angeifunua, basi nuru ya uso wake ingeunguza viumbe vyote ambacho inafikia. "Na Kitabu" cha matendo "kitawekwa hapo" na kikaendezwa ili yasomwe matendo mema na mabaya yaliyo ndani yake. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na kitawekwa kitabu. Basi utawaona wakosefu wanavyoogopa kwa yale yaliomo humo. Na watasema: Ole wetu! Kitabu hichi kina nini! Hakiachi dogo wala kubwa ila huliandika? Na watayakuta yote waliyoyatenda yamehudhuria hapo. Na Mola wako Mlezi hamdhulumu yeyote." Na kwa sababu ya uadilifu kamili na usawa, mtendaji ataambiwa: "Soma kitabu chako! Nafsi yako inakutosha leo kukuhesabu." "Na wataletwa Manabii" ili waulizwe kama walifikisha ujumbe, na kuhusu kaumu zao, na washuhudie juu yao "mashahidi" kutoka kwa Malaika, viungo na ardhi. "Na patahukumiwa baina yao kwa haki" na uadilifu kamili na mkuu. Kwa sababu ni hesabu itokayo kwa yule asiyedhulumu hata uzito wa chembe, ambaye amekidhibiti kila kitu, ambaye Kitabu chake - ambacho ni Ubao Uliohifadhiwa - kimedhibiti yote waliyoyafanya, na waandishi watukufu wasiomuasi Mola wao Mlezi, waliandika yote ambayo viumbe waliyafanya, na mashahidi waadilifu zaidi walishuhudia hukumu hiyo. Kwa hivyo, akahukumu kulingana na hayo Yule ambaye anajua kiasi cha matendo na kiasi cha thawabu na adhabu ambazo matendo hayo yanastahiki. Basi atafanya hukumu ambayo viumbe vitaikiri, na vitamkiria Mwenyezi Mungu sifa njema na uadilifu. Kwa hukumu hiyo watatambua ukuu wake, elimu yake, hekima yake na rehema yake, mambo ambayo nyoyo zao hazijawahi kuyafikiria, na ambayo ndimi zao haziwezi kuyaelezea.