سیدھے مواد پر جائیں
Tafsir As-Saadi - Swahili · Al-Ghaafir
سورت 40

Al-Ghaafir

یہ تفسیر السعدی کا ایک ترجمہ ہے جیسا IslamHouse.com اسے saadi.islamenc.com پر شائع کرتا ہے، اس سائٹ کے صفحات سے لیا گیا۔ سائٹ یہ نہیں بتاتی کہ اس کا ترجمہ کس نے کیا اور وہ کس چھپے ہوئے ایڈیشن کی پیروی کرتا ہے، اور اس کا متن لینے کی کوئی شرائط بیان نہیں کرتی، اس لیے اسے دکھانے کا حق تصدیق شدہ نہیں۔ کسی نے اسے چھپی ہوئی کتاب سے نہیں ملایا اور کسی عالم نے اس کا جائزہ نہیں لیا۔ ہر حصہ ان آیات کے ساتھ ہے جن پر وہ تبصرہ کرتا ہے، اور وہ آیات Tanzil کا قرآنی متن ہیں، جیسا وہاں ہے؛ جس آیت کی سائٹ اپنی الگ تفسیر نہیں دیتی وہ اپنے سے پہلے کے حصے کے ساتھ ہوتی ہے، اور فہرست ایسی ہر آیت کا نام لیتی ہے۔ سبیل نے اس میں سے کچھ نہیں لکھا اور نہ اس کا ترجمہ کیا۔

متن ماخوذ ازsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)2026-10-22 کو لیا گیا

آیت 28

وَقَالَ رَجُلٌ مُّؤْمِنٌ مِّنْ ءَالِ فِرْعَوْنَ يَكْتُمُ إِيمَـٰنَهُۥٓ أَتَقْتُلُونَ رَجُلًا أَن يَقُولَ رَبِّىَ ٱللَّهُ وَقَدْ جَآءَكُم بِٱلْبَيِّنَـٰتِ مِن رَّبِّكُمْ ۖ وَإِن يَكُ كَـٰذِبًا فَعَلَيْهِ كَذِبُهُۥ ۖ وَإِن يَكُ صَادِقًا يُصِبْكُم بَعْضُ ٱلَّذِى يَعِدُكُمْ ۖ إِنَّ ٱللَّهَ لَا يَهْدِى مَنْ هُوَ مُسْرِفٌ كَذَّابٌ 28

{28} Miongoni mwa visababu hivyo, ni huyu mwanamume Muumini ambaye anatoka katika familia ya Firauni kutoka katika nyumba ya ufalme, ambaye ililazimu awe katika watu wanaosikizwa maneno yao, hasa ikiwa anadhihirisha kwamba anaafikiana nao, lakini akaficha imani yake. Mara nyingi, wao humzingatia sana kushinda namna ambayo wangemzingatia ikiwa angewahalifu kwa dhahiri. Kama vile Mwenyezi Mungu alivyomzuilia Mtume wake Muhammad - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - kwa ami yake, Abu Talib kutokana na Maqureishi; kwa vile Abu Talib alikuwa mkubwa miongoni mwao na alikuwa anaafikiana nao katika dini yao. Na ikiwa angekuwa Mwislamu, basi hangeweza kumzuilia hivyo. Basi mwanamume huyo Muumini aliyewezeshwa na Mwenyezi Mungu, mwenye akili nzuri, mwenye azimio mathubuti, akasema akikemea vitendo vya watu wake na ubaya mkubwa wa yale waliyoyadhamiria kufanya: "Mtamuua mtu kwa sababu anasema Mola wangu Mlezi ni Mwenyezi Mungu?" Na kauli hii hakuisema bure tu bila hoja na msingi wowote, ndiyo maana akasema: "Na hali naye amekukujieni na hoja zilizowazi kutoka kwa Mola wenu Mlezi." Kwa sababu hoja hizo za wazi wazi alizowaletea zilidhihirika baina yao hata kwa wadogo na wazee. Kwa hivyo, hili haliwezi kuwa ndiyo sababu ya kumuua. Kwa nini hamkubatilisha kwanza haki aliyokuja nayo, na akaikabili hoja kwa hoja nyingine yenye kuipinga hoja yake, kisha baada ya hapo mkaangalia je, inaruhusika kumuuwa ikiwa mtamshinda kwa hoja au la? Lakini sasa kwa kuwa hoja yake imedhihirika na uthibitisho wake ukashinda kati yenu, na kumuuwa kuna njia ndefu ya jangwani ambayo zinakatikia hapo shingo za vipando. Kisha akawaambia maneno ya kiakili ambayo yanamshawishi kila mwenye akili nzuri kwa namna yoyote ile. Akasema: "Na akiwa yeye mwongo, basi uwongo wake ni juu yake mwenyewe. Na akiwa mkweli, yatakufikieni baadhi ya hayo anayokuahidini." Yaani, Musa yuko baina ya mambo mawili: ima ni mwongo katika madai yake hayo au ni mkweli. Ikiwa ni mwongo, basi uwongo wake huo uko juu yake, na madhara yake ni juu yake tu, hayatawapata madhara yoyote katika hilo kwa vile mlikataa kumuitikia na kumsadiki. Na kama ni mkweli, na ilhali amekukujieni na hoja zilizo wazi na akakwambieni kwamba msipomuitikia, basi Mwenyezi Mungu atakuadhibuni kwa adhabu ya duniani na adhabu nyingine Akhera, basi lazima yatawapata baadhi ya hayo anayokuahidini, ambayo ni adhabu ya duniani. Haya ni kutokana na akili yake nzuri na upole wake katika kumtetea Musa. Ambapo alikuja na jibu hili, ambalo halikuwachanganya, na akalifanya jambo hilo kuwa kati ya hali hizo mbili na kwamba katika makadirio yote, kumuua kulikuwa ni upumbavu na ujinga. Kisha akahami - Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, amghufirie na amrehemu - kwenye jambo ambalo liko juu zaidi ya hilo na kubainisha kwamba Musa yuko karibu na haki. Akasema, "Hakika Mwenyezi Mungu hamwongoi apindukiaye mipaka" kwa kuiacha haki na kuishika batili, "mwongo mkubwa," kwa kumnasibishia Mwenyezi Mungu hayo aliyopitiliza mipaka ndani yake. Huyu, Mwenyezi Mungu hawezi kumwongoa kufikia njia iliyosawa. Si katika maana yake wala katika ushahidi wake, wala hawezeshwi kufikia njia iliyonyooka. Yaani, tayari mmeshayaona yale ambayo Musa anayalingania ya haki na kile ambacho Mwenyezi Mungu alimuongoa kukieleza miongoni mwa hoja za kiakili na mambo ya kimiujiza ya mbinguni. Yule ambaye ameongoka hivi, hawezi kuwa katika wavukao mipaka wala mwongo. Huu ni ushahidi juu ya ukamilifu wa elimu yake, akili yake na kumjua kwake vyema Mola wake Mlezi.