Al-Baqara
Hii ni tarjama ya tafsiri ya as-Saʿdī kama IslamHouse.com inavyoichapisha katika saadi.islamenc.com, iliyosomwa kutoka kurasa za tovuti hiyo. Tovuti haisemi ni nani aliyeitafsiri kwa lugha nyingine wala inafuata toleo gani lililochapishwa, na haitaji masharti ya kuchukua matini yake, kwa hiyo haki ya kuionyesha haijathibitishwa. Hakuna aliyeilinganisha na kitabu kilichochapishwa, na hakuna mwanazuoni aliyeihakiki. Kila kifungu kipo kando ya aya inazozifafanua, ambazo ni matini ya Qur’ani ya Tanzil, inavyoonekana huko; aya ambayo tovuti haitoi ufafanuzi wake yenyewe inakaa pamoja na kifungu kilichotangulia, na faharasa inataja kila aya ya aina hiyo. Sabīl haikuandika wala kutafsiri kwa lugha nyingine chochote kati yake.
Maandishi kutokasaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)ilichukuliwa 2026-10-22
وَلَنَبْلُوَنَّكُم بِشَىْءٍ مِّنَ ٱلْخَوْفِ وَٱلْجُوعِ وَنَقْصٍ مِّنَ ٱلْأَمْوَٰلِ وَٱلْأَنفُسِ وَٱلثَّمَرَٰتِ ۗ وَبَشِّرِ ٱلصَّـٰبِرِينَ 155
(155) Mwenyezi Mungu alijulisha kwamba ni lazima atawatia waja wake mitihani, ili apambanuke mkweli na mwongo, na asiyeridhia na mwenye subira. Na huu ndio mwendo wake Mtukufu katika waja wake. Kwa sababu, ikiwa raha itaendelea kwa watu wa imani, na matatizo yasiwepo pamoja nayo (hiyo raha), basi mchanganyiko ungetokea, ambao ni ufisadi. Na hekima ya Mwenyezi Mungu inahitaji kuwapambanua watu wema kutokana na watu waovu. Hii ndiyo faida ya matatizo, na sio kuondoa yale waliyo nayo Waumini ya imani, wala kuwatoa katika dini yao; kwani Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuipoteza imani ya Waumini. Basi akajulisha katika Aya hii kuwa atawajaribu waja wake, “kwa chembe ya hofu” kutoka kwa madui, “na njaa.” Yaani kitu kichache katika mawili hayo. Kwa sababu, lau kuwa angewatia hofu au njaa yote, basi wangeangamia. Na matatizo yanatakasa, wala hayaangamizi. “Na upungufu wa mali.” Na hili linajumuisha upungufu wote unaoipata mali kama vile majanga ya mbinguni, na kuzama, na kupotea. Na mali kuchukuliwa na madhalimu kama vile wafalme madhalimu na majambazi wa barabarani na mengineyo. “Na watu,” yani kuondoka kwa wapendwa miongoni mwa watoto, na jamaa, na marafiki, na aina za magonjwa katika mwili wa mja au mwili wa ampendaye. “Na mazao” yani nafaka, matunda ya mitende, na miti yote, na mboga kwa mvua ya mawe, au moto, au janga kutoka mbinguni kama vile nzige na mfano wake. Kwa hivyo, haya mambo ni lazima yatokee, kwa sababu Mwenye elimu, Mwenye habari, alijulisha kuyahusu, na yakatokea kama alivyojulisha. Basi yanapotokea, watu hugawanyika katika makundi mawili: wenye huzuni na wenye subira. Basi mwenye kuhuzunika, anapata misiba miwili: kupoteza akipendacho, ambacho ni kuwepo kwa huu msiba, na kupoteza kilicho kikubwa kuliko hicho. Ambacho ni malipo ya kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu ya kuwa na subira, kwa hivyo akapata hasara na kunyimwa, na kupunguka kwa kile alichokuwa nacho katika imani. Na akapoteza subira, kuridhia, na shukrani, na akapata kukasirika kunakoashiria ukubwa wa huo upungufu. Ama yule ambaye Mwenyezi Mungu amemwezesha kuwa na subira misiba hii inapotokea, hivyo akajizuia kutoridhika katika kauli na vitendo. Na akatarajia malipo yake kwa Mwenyezi Mungu, na akajua kwamba atakayoyapata miongoni mwa malipo kwa subira yake ni makubwa kuliko msiba uliompata. Bali msiba huo unakuwa neema kwake kwa sababu unakuwa njia ya kupata kilicho bora zaidi kwake na chenye manufaa zaidi kuliko msiba huo. Kwa kuwa ameshatekeleza amri ya Mwenyezi Mungu na akapata malipo mazuri. Ndio maana Mwenyezi Mungu akasema: “Na wabashirie wanaosubiri,” yaani wape habari njema ya kwamba watalipwa ujira wao kamili bila ya hisabu. Hivyo basi, wenye subira ndio waliopata bishara kubwa, na kipawa kikubwa. Kisha akawaeleza kwa kauli yake: