Skip to content
Tafsir As-Saadi - Swahili · Al-Maaida
Sūrah 5

Al-Maaida

This is a translation of Tafsīr as-Saʿdī as IslamHouse.com publishes it at saadi.islamenc.com, read from that site’s pages. The site does not say who translated it or which printed edition it follows, and states no terms for taking its text, so the right to show it is not verified. Nobody has compared it with a printed book, and no scholar has reviewed it. Each passage stands beside the verses it comments on, which are the Qur’ān text of Tanzil, shown as it is there; a verse the site gives no commentary of its own stands with the passage before it, and the index names each such verse. Sabīl did not write or translate any of it.

Text fromsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)taken 2026-10-22

Verse 33

إِنَّمَا جَزَٰٓؤُا۟ ٱلَّذِينَ يُحَارِبُونَ ٱللَّهَ وَرَسُولَهُۥ وَيَسْعَوْنَ فِى ٱلْأَرْضِ فَسَادًا أَن يُقَتَّلُوٓا۟ أَوْ يُصَلَّبُوٓا۟ أَوْ تُقَطَّعَ أَيْدِيهِمْ وَأَرْجُلُهُم مِّنْ خِلَـٰفٍ أَوْ يُنفَوْا۟ مِنَ ٱلْأَرْضِ ۚ ذَٰلِكَ لَهُمْ خِزْىٌ فِى ٱلدُّنْيَا ۖ وَلَهُمْ فِى ٱلْـَٔاخِرَةِ عَذَابٌ عَظِيمٌ 33

{33} Wale wanaompiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake ni wale waliomfanyia uadui na wakaeneza uharibifu katika ardhi kwa ukafiri, na kuua, na kuchukua mali, na kutia hofu kwenye njia. Na lililo mashuhuri katika hukumu za majambazi wa barabarani ambao wanawavamia watu vijijini na majangwani, na kuwanyang'anya mali zao, na kuwaua na kuwahofisha, basi watu wakajizuia kufuata njia ambazo wao wako; kwa hivyo zikawa njia hizo zimekatika kwa hilo. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu akajulisha kwamba malipo yao na adhabu yao wakati wanapotekelezewa adhabu maalum ya kisheria ni kwamba wafanyiwe moja ya mambo mbalimbali. Na Wafasiri wamehitalifiana kuhusu je, hayo mambo yanaweza kufanywa baadhi yake na kuachwa baadhi yake? Na kwamba, kila jambazi wa njiani anafanyiwa na imamu au mwakilishi wake kile anachoona kinafaa katika mambo haya yaliyotajwa? Na hii ndiyo maana ya dhahiri ya andiko hili. Au kwamba adhabu yao inakuwa kulingana na uhalifu wao. Kwa hivyo kila uhalifu una fungu linalolingana nao. Kama Aya inavyoonyesha hilo kwa hekima yake na kuafikiana kwake na hekima ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na kwamba ikiwa wataua na wakachukua mali, basi inalazimu kuwaua na kuwasulubisha, mpaka habari yao ienee, na wafedheheshwe, na wakomeke wengineo. Na ikiwa waliua lakini hawakuchukua mali yoyote, basi inalazimu kuwaua tu. Na ikiwa walichukua mali na hawakuuwa, basi inalazimu kuikata Mikono yao na miguu yao kwa kinyume. Mkono wa kulia na mguu wa kushoto. Na wakiwahofisha watu, na hawakuuwa, wala hawakuchukua mali, basi watafukuzwa kutoka katika nchi, na hawataachwa kutafuta kimbilio katika nchi yoyote mpaka toba yao ionekane dhahiri. Na hii ni kauli ya Ibn Abbas, Mwenyezi Mungu amwiye radhi, na maimamu wengi pamoja na kuwepo tofauti katika baadhi ya maelezo ya kina. "Hiyo" [adhabu] "kwao ni hizaya katika dunia" yani fedheha na kuaibishwa, "katika Akhera wana adhabu kubwa". Basi hili likaashiria kuwa kuzuilia njia ni miongoni mwa madhambi makubwa zaidi yanayopelekea kupata fedheha ya duniani na adhabu ya Akhera. Na kwamba mwenye kufanya hilo anampiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na ikiwa ndivyo ilivyo kwa uzito wa uhalifu huu, basi inajulikana kuwa kuitakasa ardhi kutokana na waharibifu, na kuweka amani katika njia na barabara kutokana na kuua, na kuchukua mali, na kuwahofisha watu ni miongoni mwa matendo mazuri makubwa zaidi, na utiifu mtukufu zaidi. Na kwamba ni kuifanya ardhi kutengenea, kama vile kinyume chake ni uharibifu katika ardhi.