Skip to content
Tafsir As-Saadi - Swahili · Al-Baqara
Sūrah 2

Al-Baqara

This is a translation of Tafsīr as-Saʿdī as IslamHouse.com publishes it at saadi.islamenc.com, read from that site’s pages. The site does not say who translated it or which printed edition it follows, and states no terms for taking its text, so the right to show it is not verified. Nobody has compared it with a printed book, and no scholar has reviewed it. Each passage stands beside the verses it comments on, which are the Qur’ān text of Tanzil, shown as it is there; a verse the site gives no commentary of its own stands with the passage before it, and the index names each such verse. Sabīl did not write or translate any of it.

Text fromsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)taken 2026-10-22

Verse 91

وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ ءَامِنُوا۟ بِمَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ قَالُوا۟ نُؤْمِنُ بِمَآ أُنزِلَ عَلَيْنَا وَيَكْفُرُونَ بِمَا وَرَآءَهُۥ وَهُوَ ٱلْحَقُّ مُصَدِّقًا لِّمَا مَعَهُمْ ۗ قُلْ فَلِمَ تَقْتُلُونَ أَنۢبِيَآءَ ٱللَّهِ مِن قَبْلُ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ 91

(91) Yani Mayahudi wanapoamrishwa kuamini aliyoteremsha Mwenyezi Mungu juu ya Mtume wake, nayo ni Qur-ani, wanajivuna na kufanya jeuri, na "Wao husema: Tunaamini tuliyo teremshiwa sisi. Na huyakataa yasiyokuwa hayo." Katika vitabu vinginevyo, pamoja na kwamba wajibu ni kwamba waamini aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu yote, sawa yawe yaliteremshwa kwao au kwa wasiokuwa wao. Na hii ndiyo imani yenye manufaa. Kuamini aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu kwa Mitume wote [wa Mwenyezi Mungu]. Na ama kutofautisha baina ya Mitume na Vitabu, na kudai kuamini baadhi yake na sio baadhi yake, hili sio imani, bali ndio ukafiri wenyewe. Na ndiyo maana Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema "Hakika wale wanaomkataa Mwenyezi Mungu na Mitume wake, na wanataka kufarikisha baina ya Mwenyezi Mungu na Mitume wake, kwa kusema: Wengine tunawaamini na wengine tunawakataa. Na wanataka kushika njia iliyo katikati ya haya, hao ndio makafiri kweli." Ndio maana Mwenyezi Mungu Mwenye baraka, Mtukufu aliwajibu hapa kwa jawabu la kutosheleza, na akalazimisha kulazimisha ambako hawana njia ya kutokea. Akajibu kukufuru kwao Qur-ani kwa mambo mawili, akasema: "Na hali ya kuwa hii ndiyo haki." Basi ikiwa ni haki katika yote iliyojumuisha katika habari, na maamrisho, na makatazo, nayo inatoka kwa Mola wao Mlezi; basi kuikufuru baada ya hilo ni kumkufuru Mwenyezi Mungu na kuikufuru haki ambayo aliteremsha. Kisha akasema "inayothibitisha yale waliyo nayo wao" yani inayoafikiana nayo katika kila iliyoashiria katika haki, na yenye kuyalinda. Basi kwa nini mnaamini yaliyoteremshwa juu yenu na mnakikataa kilicho sawa nayo? Je, huu sio tu ushabiki na kufuata matamanio, badala ya uwongofu? Vilevile, kwa kuwa Qur-ani inasadikisha yale waliyo nayo inalazimu kuwa ni hoja kwao juu ya usahihi wa yale yaliyomo mikononi mwao miongoni mwa vitabu, kwa hivyo hawana njia ya kuyathibitisha isipokuwa kwa hiyo (Qur-ani). Na wakiikufuru na kuikanusha, wanakuwa katika nafasi ya yule aliyedai madai kwa hoja na ushahidi, ambavyo hana vingine visivyokuwa hivyo, na wala madai yake hayawezi kutimia isipokuwa kwa ushahidi wake kusalimika. Kisha akaujia huo ushahidi wake na hoja yake na akavikashifu na akavikadhibisha. Je, huu si upumbavu na wazimu tu? Basi ukawa kuikufuru kwao Qur-ani ni kukufuru yale waliyo nayo mikononi mwao, na kuyapinga. Kisha Mwenyezi Mungu Mtukufu akawapinga juu ya hayo madai yao kwamba wanaamini yaliyoteremshwa kwao kwa kauli yake. "Sema," uwaambie: "Mbona mliwauwa Manabii wa Mwenyezi Mungu hapo zamani ikiwa kweli mlikuwa Waumini?"