Al-Baqara
This is a translation of Tafsīr as-Saʿdī as IslamHouse.com publishes it at saadi.islamenc.com, read from that site’s pages. The site does not say who translated it or which printed edition it follows, and states no terms for taking its text, so the right to show it is not verified. Nobody has compared it with a printed book, and no scholar has reviewed it. Each passage stands beside the verses it comments on, which are the Qur’ān text of Tanzil, shown as it is there; a verse the site gives no commentary of its own stands with the passage before it, and the index names each such verse. Sabīl did not write or translate any of it.
Text fromsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)taken 2026-10-22
ثُمَّ قَسَتْ قُلُوبُكُم مِّنۢ بَعْدِ ذَٰلِكَ فَهِىَ كَٱلْحِجَارَةِ أَوْ أَشَدُّ قَسْوَةً ۚ وَإِنَّ مِنَ ٱلْحِجَارَةِ لَمَا يَتَفَجَّرُ مِنْهُ ٱلْأَنْهَـٰرُ ۚ وَإِنَّ مِنْهَا لَمَا يَشَّقَّقُ فَيَخْرُجُ مِنْهُ ٱلْمَآءُ ۚ وَإِنَّ مِنْهَا لَمَا يَهْبِطُ مِنْ خَشْيَةِ ٱللَّهِ ۗ وَمَا ٱللَّهُ بِغَـٰفِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ 74
(74) "Kisha nyoyo zenu zikawa ngumu" yani zikawa ngumu na sugu ambazo haziathiriwi na mawaidha "baada ya hayo" yani baada ya Mwenyezi Mungu kuwapa neema kubwa na akawaonyesha ishara. Na wala nyoyo zenu hazikufaa kuwa ngumu, kwa sababu mliyoyaona ni katika yale yanayolazimu upole wa nyoyo na kufuata kwake amri. Kisha akaueleza ugumu wake kuwa ni "kama mawe" ambayo huwa magumu zaidi kuliko chuma. Kwa sababu, chuma na risasi vikiyeyuka katika moto, vinayeyuka, kinyume na mawe. Na kauli yake "au ngumu zaidi" yani hazipunguki chini ya ugumu wa mawe. Na "au" hapa haimaanishi "bali" Kisha akataja ubora wa mawe juu ya nyoyo zao. Akasema "kwani kuna mawe yanayotimbuka mito, na kuna mengine yanayopasuka yakatoka maji ndani yake, na kuna mengine huanguka kwa sababu ya kumhofu Mwenyezi Mungu." Na kwa sababu ya mambo haya, mawe ni bora zaidi kuliko nyoyo zenu. Kisha Mwenyezi Mungu Mtukufu akawatishia kwa tishio kali kabisa, akasema "Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na mnayoyafanya." Bali Yeye anayajua na anayahifadhi, madogo yake na makubwa yake, na atawalipa kwa hayo, malipo kamili na timilifu. Na jua ya kwamba wengi katika wafasiri - Mwenyezi Mungu awarehemu - wamezijaza kwa wingi tafsiri zao kwa visa vya Wana wa Israili, na wakaviteremshia Aya za Qur-ani, na wakavifanya kuwa tafsiri ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu, huku wakiichukua kama hoja kauli yake (Mtume) rehema na amani ziwe juu yake. "Simulieni kutoka kwa Wana wa Israili, wala hakuna ubaya." Na ninachokiona mimi ni kuwa, hata ikiruhusika kuzisimulia hadithi zao kwa namna ambayo zinakuwa pekee yake bila ya kuziunganisha wala kuziteremsha juu ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu, basi hairuhusiki kabisa kuzifanya kuwa tafsiri ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu; ikiwa hazikupokewa kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani ziwe juu yake. Na hilo ni kwa sababu daraja yake ni kama alivyosema (Mtume) rehema na amani ziwe juu yake. "Msiwasadiki watu wa Kitabu wala msiwakadhibishe.” Hivyo basi, ikiwa daraja yake ni kwamba zina shaka ndani yake, na jambo linalojulikana kwa lazima katika dini ya Uislamu ni kwamba ni lazima kuiamini Qur-ani. Na kuwa na uhakika na maneno na maana zake, basi hairuhusiki kuzifanya hadithi hizo - zinazosimuliwa kwa riwaya zisizojulikana (ambazo zinadhaniwa sana kwamba ni za uongo), au zenye uongo katika nyingi zake - kuwa maana ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa hakika. Na wala hakuna yeyote mwenye shaka juu ya hili. Lakini kwa sababu ya kughafilika katika haya, yaliyotokea yalitokea, na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuwezesha.