Skip to content
Tafsir As-Saadi - Swahili · An-Nahl
Sūrah 16

An-Nahl

This is a translation of Tafsīr as-Saʿdī as IslamHouse.com publishes it at saadi.islamenc.com, read from that site’s pages. The site does not say who translated it or which printed edition it follows, and states no terms for taking its text, so the right to show it is not verified. Nobody has compared it with a printed book, and no scholar has reviewed it. Each passage stands beside the verses it comments on, which are the Qur’ān text of Tanzil, shown as it is there; a verse the site gives no commentary of its own stands with the passage before it, and the index names each such verse. Sabīl did not write or translate any of it.

Text fromsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)taken 2026-10-22

Verses 57–59

وَيَجْعَلُونَ لِلَّهِ ٱلْبَنَـٰتِ سُبْحَـٰنَهُۥ ۙ وَلَهُم مَّا يَشْتَهُونَ 57 وَإِذَا بُشِّرَ أَحَدُهُم بِٱلْأُنثَىٰ ظَلَّ وَجْهُهُۥ مُسْوَدًّا وَهُوَ كَظِيمٌ 58 يَتَوَٰرَىٰ مِنَ ٱلْقَوْمِ مِن سُوٓءِ مَا بُشِّرَ بِهِۦٓ ۚ أَيُمْسِكُهُۥ عَلَىٰ هُونٍ أَمْ يَدُسُّهُۥ فِى ٱلتُّرَابِ ۗ أَلَا سَآءَ مَا يَحْكُمُونَ 59

{57 - 59} "Na wanamfanyia Mwenyezi Mungu ati ana mabinti" ambapo walisema hivi kuhusu malaika ambao ni waja walio karibu na Mwenyezi Mungu: Wao ni mabinti wa Mwenyezi Mungu, "Na wao wenyewe, ati ndiyo wawe na hayo wanayoyatamani!" Yaani, wao wenyewe wanajitakia wana wa kiume, kiasi kwamba wanawachukia sana mabinti. Kwa hivyo mmoja wao alikuwa "akibashiriwa kwa msichana, uso wake unasalia umesawijika" kwa sababu ya dhiki iliyoyapata. "Na akajizuia mno huzuni;" yaani, anajizuia mno huzuni na majuto anapobashiriwa kuzaliwa mwana wa kike, kiasi kwamba anafedheheshwa mbele ya wenzake na anajificha asionekane na watu kwa ubaya wa yule aliyebashiriwa! Kisha anafikiria kwa mawazo yake mabovu kuhusu atakalomfanyia binti ambaye amebashiriwa."Je, akae naye juu ya fedheha hiyo au amfukie udongoni" hali akiwa hai? Nako ni kule kuwauwa mabinti wachanga ambako Mwenyezi Mungu aliwakashifu washirikina juu yake. "Tazama, ni ubaya mno wanavyohukumu!" Ambapo walimuelezea Mwenyezi Mungu kwa njia ambayo haiufailii utukufu wake kwa kumnasibishia mwana. Tena hilo halikuwatosha hadi walipomnasibisha na sehemu mbaya zaidi kati ya sehemu hizo mbili, ambayo ni wanawake ambao wao wenyewe hawawapendi mno na wanawachukia. Basi vipi wanawanasibisha kwa Mwenyezi Mungu? Basi hukumu mbaya zaidi ni hukumu yao hiyo.