An-Nisaa
Kani waa tarjumaad tafsiirka as-Saʿdī sida IslamHouse.com ugu daabacdo saadi.islamenc.com, oo laga akhriyay bogagga goobtaas. Goobtu ma sheegayso cidda tarjuntay ama daabacaadda la daabacay ee ay raacayso, mana sheegayso shuruudo qaadashada qoraalkeeda ah, sidaas darteed xaqa muujinteeda lama xaqiijin. Qofna ma barbardhigin buug la daabacay, aqoonyahanna ma dib u eegin. Qayb kasta waxay ag taagan tahay aayadaha ay ka hadlayso, kuwaas oo ah qoraalka Quraanka ee Tanzil, sida uu ugu yaal halkaas; aayad goobtu aanay faallo u gaar ah ka bixin waxay la taagan tahay qaybta ka horraysa, tusmaduna waxay magacaabaysaa aayad kasta oo caynkaas ah. Sabīl wax ka mid ah ma qorin, mana tarjumin.
Qoraalka waxaa laga helaysaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)la qaaday 2026-10-22
وَإِذَا كُنتَ فِيهِمْ فَأَقَمْتَ لَهُمُ ٱلصَّلَوٰةَ فَلْتَقُمْ طَآئِفَةٌ مِّنْهُم مَّعَكَ وَلْيَأْخُذُوٓا۟ أَسْلِحَتَهُمْ فَإِذَا سَجَدُوا۟ فَلْيَكُونُوا۟ مِن وَرَآئِكُمْ وَلْتَأْتِ طَآئِفَةٌ أُخْرَىٰ لَمْ يُصَلُّوا۟ فَلْيُصَلُّوا۟ مَعَكَ وَلْيَأْخُذُوا۟ حِذْرَهُمْ وَأَسْلِحَتَهُمْ ۗ وَدَّ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ لَوْ تَغْفُلُونَ عَنْ أَسْلِحَتِكُمْ وَأَمْتِعَتِكُمْ فَيَمِيلُونَ عَلَيْكُم مَّيْلَةً وَٰحِدَةً ۚ وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِن كَانَ بِكُمْ أَذًى مِّن مَّطَرٍ أَوْ كُنتُم مَّرْضَىٰٓ أَن تَضَعُوٓا۟ أَسْلِحَتَكُمْ ۖ وَخُذُوا۟ حِذْرَكُمْ ۗ إِنَّ ٱللَّهَ أَعَدَّ لِلْكَـٰفِرِينَ عَذَابًا مُّهِينًا 102
{102} Na ndio maana akaja na namna ya Swala ya hofu baada yake kwa kauli yake. “Na unapokuwa miongoni mwao, na ukawasimamishia Swala” Yani ukawaongoza katika kusimamisha Swala pamoja nao na kukamilisha yale yanayotakiwa ndani yake, na yanalazimika wayafanye yanayofaa wewe na wao. Kisha akaeleza hayo kwa kauli yake, “basi kundi moja miongoni mwao lisimame pamoja nawe.” Yani kundi lingine lisimame kuwaelekea adui, kama yanaashiria hilo yafuatayo. “Na watakapomaliza kusujudu” yani wale walio pamoja nawe. Yani wanapomaliza Swala yao. Na alitumia neno kusujudu badala ya Swala ili kuashiria fadhila ya kusujudu, na kwamba ni nguzo katika nguzo zake, bali hiyo ndiyo kubwa zaidi. “Basi na wawe nyuma yenu, na lije kundi lingine ambalo halijaswali.” Nao ndio wale waliosimama kwa kuwaelekea maadui, “na waswali pamoja nawe.” Na hilo linaashiria kuwa imamu anabaki akingojea kundi la pili baada ya kundi la kwanza kuondoka. Na wanapofika, anawaswalisha kile kilichobaki katika swala yake, kisha atakaa akiwangoja mpaka wamalize swala yao, kisha atatoa salamu ya kumaliza swala akiwa pamoja nao. Na ni moja ya namna za kuswali swala ya hofu. Na imethibiti kutoka kwa Nabii – rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake – namna nyingi, na zote zinaruhusika. Na Aya hii inaonyesha kwamba swala ya jamaa ni faradhi juu ya kila mtu kwa njia mbili: Moja yake ni kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu aliiamuru katika hali hii ngumu, wakati wa hofu kubwa juu ya maadui na tahadhari juu ya mashambulizi yao. Na ikiwa aliiwajibisha katika hali hii ngumu, basi kuilazimisha katika hali ya utulivu na usalama inastahiki zaidi na inafaa zaidi. Ya pili ni kwamba wale wanaoswali swala ya hofu huacha ndani yake masharti mengi na yale yanayolazimika, na wanasamehewa ndani yake vitendo vingi vyenye kubatilisha swala katika isiyokuwa Swala hii. Na hilo si isipokuwa kusisitiza ufaradhi wa swala ya jamaa. Kwa sababu, hakuna mgongano kati ya wajibu na yenye kupendekezwa. Na lau si uwajibu wa swala ya jamaa, basi hayangeachwa mambo haya ya lazima kwa ajili yake. Aya hii tukufu inaashiria kuwa ni vyema na bora zaidi kwao kuswali pamoja na imamu mmoja, hata kama hilo litahusisha kukiuka jambo ambalo halitaharibu kitu iwapo wataiswali kwa maimamu kadhaa. Na hilo ni kwa ajili ya kuunganisha neno la Waislamu, na kukubaliana kwao, na kutolitenganisha neno lao, na ili hili liwe lenye kuweka haiba zaidi katika mioyo ya maadui zao. Na Mola Mtukufu aliamrisha zichukuliwe silaha na kutahadhari katika swala ya hofu. Na hili ijapokuwa ndani yake kuna harakati na kujishughulisha nje ya baadhi ya hali za swala, lakini ndani yake kuna masilahi makubwa zaidi. Nayo ni kuchanganya kati ya Swala, na Jihadi, na kujihadhari na maadui ambao wana nia kubwa sana ya kuwaumiza Waislamu na kuwashambulia wao na mizigo yao. Na ndiyo maana Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema, “Walipenda wale waliokufuru lau mghafilike na silaha zenu na mizigo yenu ili wawavamie mvamio wa mara moja.” Kisha Mwenyezi Mungu akamkubalia mwenye udhuru kama vile maradhi au mvua kwamba aweke silaha yake, lakini awe mwenye kuchukua tahadhari. Akasema, “Wala hakuna ubaya juu yenu ikiwa mnaona udhia kwa sababu ya mvua au mkawa wagonjwa, mkaziweka silaha zenu. Na chukueni hadhari yenu. Hakika, Mwenyezi Mungu amewaandalia makafiri adhabu ya kudunisha.” Na katika adhabu ya kudunisha ni kile ambacho Mwenyezi Mungu aliliamrisha kundi lake la Waumini na wale wanaoinusuru dini yake, wanaomfanyia Yeye tu dini kwamba wawaue, na kupigana nao popote watakapowakuta, na kuwakamata, na wawazingire, na wavizie katika kila njia, na watahadhari nao katika kila hali, na wala wasinghafilike nao kwa kuogopa makafiri wasije wakayapata baadhi ya wanayoyataka kutoka kwao. Basi ni za Mwenyezi Mungu himidi njema zote kubwa, na sifa kwa yale aliyowaneemesha kwayo Waumini na akawaunga mkono kwa msaada wake, na mafundisho yake, ambayo ikiwa watayafuata kwa namna ya ukamilifu, basi bendera yao haitaweza kushindwa kamwe. Na hakuna adui yeyote anayeweza kuwa juu yao wakati wowote ule. Na kauli yake, "Na watakapomaliza kusujudu, basi na wawe nyuma yenu" inaashiria kuwa kundi hili linapaswa kukamilisha swala yake yote kabla ya kwenda kwenye sehemu ya walinzi. Na kwamba Mtume – rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake – anabaki akingojea kundi lile lingine kabla ya kutoa salamu. Kwa sababu kwanza alitaja kuwa kundi moja lisimame pamoja naye. Kwa hivyo akajulisha kuhusu kuandamana kwao pamoja naye. Kisha akafungamanisha kitendo hicho tena na wao tu, na si Mtume. Kwa hivyo hilo likaashiria yale tuliyoyataja. Na katika kauli Yake, “na lije kundi lingine ambalo halijaswali, na waswali pamoja nawe," kuna ushahidi kuwa kundi la kwanza limeshaswali. Na kwamba swala yote ya kundi la pili inakuwa pamoja na imamu kiuhakika katika rakaa yao ya kwanza, na kihukumu katika rakaa yao ya mwisho. Kwa hivyo hilo likalazimu imamu awangojee mpaka wamalize swala yao, kisha atoe salamu akiwa pamoja nao. Na hili linaonekana wazi kwa mwenye kutafakari.