Faatir
Ini ialah terjemahan Tafsir as-Saʿdī seperti yang diterbitkan oleh IslamHouse.com di saadi.islamenc.com, dibaca daripada halaman-halaman laman itu. Laman itu tidak menyatakan siapa yang menterjemahkannya atau edisi cetakan mana yang diikutinya, dan tidak menyatakan syarat untuk mengambil teksnya, maka hak untuk memaparkannya belum disahkan. Belum ada sesiapa yang membandingkannya dengan buku bercetak, dan tiada ulama yang menyemaknya. Setiap bahagian berada di sisi ayat-ayat yang diulasnya, iaitu teks Al-Quran daripada Tanzil, dipaparkan seperti yang ada di sana; ayat yang tidak diberi ulasan tersendiri oleh laman itu berada bersama bahagian sebelumnya, dan indeks menamakan setiap ayat sedemikian. Sabīl tidak menulis atau menterjemahkan satu pun daripadanya.
Teks daripadasaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)diambil pada 2026-10-22
قُلْ أَرَءَيْتُمْ شُرَكَآءَكُمُ ٱلَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ ٱللَّهِ أَرُونِى مَاذَا خَلَقُوا۟ مِنَ ٱلْأَرْضِ أَمْ لَهُمْ شِرْكٌ فِى ٱلسَّمَـٰوَٰتِ أَمْ ءَاتَيْنَـٰهُمْ كِتَـٰبًا فَهُمْ عَلَىٰ بَيِّنَتٍ مِّنْهُ ۚ بَلْ إِن يَعِدُ ٱلظَّـٰلِمُونَ بَعْضُهُم بَعْضًا إِلَّا غُرُورًا 40
{40} Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema, akionyesha kutoweza kwa miungu ya washirikina na kuonyesha upungufu wao na ubatili wa ushirikina wao kwa njia zote: "Sema" ewe Mtume ukiwaambia: "Mnawaona," yaani niambieni kuhusu hawa miungu wenu wa kishirikina "mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu!" Je, wanastahiki kuombwa dua na kuabudiwa? Basi nionyesheni "wameumba sehemu gani katika ardhi?" Je, waliumba bahari yoyote, au waliumba mlima wowote, au waliumba wanyama wowote, au waliumba kitu chochote kisichokuwa na uhai? Watakiri kwamba Muumba wa vitu vyote ni Mwenyezi Mungu. Au washirika wenu hawa wana "ushirika wowote katika mbingu" katika kuziumba na kuziendesha? Watasema: Hawana ushirika wowote. Kwa hivyo, ikiwa hawakuumba chochote na hawakumshiriki Muumba katika kuumba kwake, basi kwa nini mliwaabudu na kuwaomba dua ilhali mnakiri kutokuwa kwao na uwezo? Basi ukaishia hapo ushahidi wa kiakili ulioonyesha ubatili wa kuabudiwa kwao. Kisha akataja ushahidi wa kusikia, na kwamba hilo pia haliko, na ndiyo maana akasema: "Au tumewapa Kitabu" kinachozungumzia yale waliyokuwa wakiyashirikisha; kikiwaamrisha kufanya ushirikina na kuabudu visivyokuwa Mwenyezi Mungu? "Nao kwa hicho wakawa na hoja zilizowazi katika ushirikina wao huo kupitia kitabu chao hicho kilichowateremkia kikionyesha usahihi wa kufanya ushirikina?" Si hivyo, kwani hawakuteremshiwa Kitabu chochote kabla ya Qur-ani, na wala mwonyaji yeyote hakuwahiwajia kabla ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Lakini hata kama ingechukuliwa kwamba kitabu kiliwashukia na kwamba walitumiwa Mtume, nao wakadai kwamba yeye ndiye aliyeamrisha kufanya ushirikina, basi sisi bila ya shaka tunajua kwamba ni waongo. Kwa sababu Mwenyezi Mungu alisema: "Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimfunulia ya kwamba hapana mungu isipokuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu." Basi wameafikiana Mitume wote na Vitabu vyote juu ya suala la kuwaamrisha watu kumkusudia Mwenyezi Mungu peke yake katika Dini. "Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Dini, wawe waongofu." Na ikisemwa: Iwapo ushahidi wa kiakili na wa kimaandiko ulionyesha ubatili wa ushirikina wao, basi ni nini kiliwafanya washirikina wafanye ushirikina ilhali miongoni mwao wapo watu wenye akili, werevu na wenye ufahamu mkubwa? Mwenyezi Mungu Mtukufu akajibu kwa kauli yake: "Lakini madhalimu hawaahidiani wao kwa wao ila udanganyifu tu." Yaani, hayo waliyoyafanya hawana hoja yoyote juu yake, bali hayo ni wasia waliousiana wao kwa wao, na wakapambiana wao kwa wao. Na wale waliokuja baadaye kuwaiga waliotangulia ambao walipotea.Na matumaini ambayo mashetani waliwapa na wakawapambia ubaya wa matendo yao, kwa hivyo yakakolea katika nyoyo zao na yakawa ni moja ya sifa zake.Kwa hivyo ikawa vigumu kuyatoa na kutengana nayo, kwa hivyo yakatokea yaliyotokea ya kudumu kwao katika ukafiri na ushirikina wa batili utakaotoweka.