Langkau ke kandungan
Tafsir As-Saadi - Swahili · Al-Baqara
Surah 2

Al-Baqara

Ini ialah terjemahan Tafsir as-Saʿdī seperti yang diterbitkan oleh IslamHouse.com di saadi.islamenc.com, dibaca daripada halaman-halaman laman itu. Laman itu tidak menyatakan siapa yang menterjemahkannya atau edisi cetakan mana yang diikutinya, dan tidak menyatakan syarat untuk mengambil teksnya, maka hak untuk memaparkannya belum disahkan. Belum ada sesiapa yang membandingkannya dengan buku bercetak, dan tiada ulama yang menyemaknya. Setiap bahagian berada di sisi ayat-ayat yang diulasnya, iaitu teks Al-Quran daripada Tanzil, dipaparkan seperti yang ada di sana; ayat yang tidak diberi ulasan tersendiri oleh laman itu berada bersama bahagian sebelumnya, dan indeks menamakan setiap ayat sedemikian. Sabīl tidak menulis atau menterjemahkan satu pun daripadanya.

Teks daripadasaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)diambil pada 2026-10-22

Ayat 136

قُولُوٓا۟ ءَامَنَّا بِٱللَّهِ وَمَآ أُنزِلَ إِلَيْنَا وَمَآ أُنزِلَ إِلَىٰٓ إِبْرَٰهِـۧمَ وَإِسْمَـٰعِيلَ وَإِسْحَـٰقَ وَيَعْقُوبَ وَٱلْأَسْبَاطِ وَمَآ أُوتِىَ مُوسَىٰ وَعِيسَىٰ وَمَآ أُوتِىَ ٱلنَّبِيُّونَ مِن رَّبِّهِمْ لَا نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِّنْهُمْ وَنَحْنُ لَهُۥ مُسْلِمُونَ 136

(136) Hii aya tukufu inajumuisha kila kitu ambacho ni lazima kiaminewe. Na jua ya kwamba imani ambayo ni kusadiki kikamilifu kwa moyo kwa hii misingi na kukiri kwake kunakojumuisha matendo ya nyoyo na viungo, ambako - Kwa huu mtazamo - Uislamu unaingia ndani yake; na matendo mema yote yanaingia ndani yake pia. Hivyo basi, hayo ni sehemu ya imani na athari katika athari zake. Na imani (neno) inapotajwa peke yake, yale yaliyotajwa huingia ndani yake. Na vile vile Uislamu unapoatajwa peke yake, imani huingia ndani yake. Na vinapotajwa kwa pamoja, imani huwa jina kwa yale yaliyomo ndani ya moyo kama vile kukiri na kusadiki. Nao Uislamu huwa jina kwa matendo ya nje, na kadhalika ikiwa imani na matendo mema vitatajwa kwa pamoja. Basi, kauli yake Mtukufu "Semeni nyinyi," yani kwa ndimi zenu nyoyo zikiwa zinaafikiana na ndimi juu ya hayo. Na hii ndiyo kauli kamili inayosababisha thawabu na malipo. Na kama vile kutamka kwa ulimi bila ya moyo kuamini ni unafiki na ukafiri. Basi vile vile kauli isiyokuwa na vitendo, vitendo vya moyo, hayana athari, na yana manufaa faida ndogo, ingawa mja hulipwa kwa hilo ikiwa ni la heri na yeye kimsingi anaamini. Lakini tofautisha kati ya kauli tupu, na ile (kauli) iliyofungamana na matendo ya moyo. Na katika kauli yake "Semeni nyinyi" kuna ishara ya kuiweka wazi na kuitangaza itikadi (imani), na kulingania kwayo, kwani ndiyo msingi wa dini na asasi yake. Na katika kauli yake, "Tumemuamini" na mfano wake, ambayo ndani yake kuna kitendo kinachotoka kwa umma wote kuna ishara kuwa ni lazima juu ya umma kushikamana wote na kamba ya Mwenyezi Mungu, na kuuhimiza muungano ili kulingania kwao kuwe kumoja, na matendo yao yake yameungana. Na ndani yake kuna katazo la kutengana. Na ndani yake kuna kwamba Waumini ni kama mwili mmoja. Na katika kauli yake "Semeni nyinyi: Tumemuamini Mwenyezi Mungu" hadi mwisho, kuna dalili ya kuruhusiwa mtu kujinasibishia nafsi yake imani kwa namna ya kubana. Bali ni lazima kufanya hivyo, kinyume na kauli yake "Mimi ni Muumini” na mfano wake. Kwa maana, haisemwi hivi isipokuwa kwa kuifungamanisha na mapenzi ya Mwenyezi Mungu (yani kusema in shaa Allah). Kwa sababu, ndani yake kuna kujitakasa nafsi na kujishuhudia mwenyewe kuwa na imani. Kwa hivyo, kauli yake;"tumemuamini Mwenyezi Mungu," yani kwamba Yeye yupo, Mmoja, Mpweke, mwenye kusifika kwa sifa zote za ukamilifu, aliyetakasika kutokana na kila upungufu na kasoro, anayestahiki kupwekeshwa na ibada zote, na kutomshirikisha na chochote katika hayo kwa njia yoyote ile. "Na yale tuliyoteremshiwa sisi" yanajumuisha Qur-ani na Sunnah kwa kauli yake Mtukufu. "Na Mwenyezi Mungu alikuteremshia Kitabu na hekima." Kwa hivyo, ikaingia ndani yake kuamini yale yaliyomo ndani ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume wake, miongoni mwa sifa za Muumba, sifa za Mitume wake, Siku ya Mwisho na ghaibu zilizopita na zijazo. Na kuamini yaliyomo ndani ya hayo miognoni mwa hukumu za kisheria za lazima, hukumu za adhabu na kadhalika. "Na yaliyoteremshwa kwa Ibrahim" hadi mwisho wa Aya hii, ndani yake kuna imani katika vitabu vyote vilivyoteremshwa kwa Manabii wote, na kuwaamini Manabii kwa ujumla. Na pia kindani, hasa wale waliotajwa katika Aya hii kwa sababu ya heshima yao, na kwa sababu ya kuleta kwao sheria kubwa. Hivyo basi, la wajibu katika kuamini katika Manabii na Vitabu ni kuwaamini kwa namna ya ujumla, na ya kuwaingiza wote. Kisha kile kinachojulikana kuwahusu kwa undani, ni lazima kukiamini kwa undani. Na kauli yake, "hatutofautishi baina ya yeyote katika hao," yani bali sisi tunawaamini wote. Hii ni sifa ya kipekee ya Waislamu ambayo wanasifika kwayo wao tu kando na kila anayedai kuwa kwenye dini fulani. Kwa hivyo, Mayahudi, Wakristo, Masabii na wengineo, hata kama wanadai kuwa wanaamini wanayoyaamini miongoni mwa Mitume na Vitabu, wao kwa hakika wanaamini baadhi yake; na wakakufuru baadhi yake. Kwa hivyo, kukadhibisha kwao kunabatilisha kusadiki kwao. Kwa maana, Mtume ambaye walidai kuwa walimwamini, yeye aliwasadiki Mitume wote hasa Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake. Kwa hivyo, wakimkadhibisha Muhammad, basi watakuwa wamemkadhibisha Mtume wao katika yale aliyowaambia, na hilo linakuwa kumkufuru Mtume wao. Na katika kauli yake, "na pia waliyopewa Manabii wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi." Kuna dalili ya kuwa kipawa cha dini ndicho kipawa cha uhakika, kinachohusiana na furaha ya kidunia na ya kiakhera. Hakutuamrisha tuyaamini waliyopewa Manabii katika ufalme na mali na mfano wa hayo. Bali alituamrisha tuyaamini waliyopewa katika Vitabu na sheria. Na ndani yake kuna kwamba Manabii ni wafikishaji tu kwa niaba ya Mwenyezi Mungu, na wapatanishi baina ya Mwenyezi Mungu na viumbe vyake katika kuifikisha dini yake. Hawana lao katika hili jambo. Na katika kauli yake, "kutoka kwa Mola wao Mlezi" kuna ishara kwamba kwa sababu ya ukamilifu wa uungu wake kwa waja wake, ni kwamba awateremshie Vitabu na kuwatumia Mitume. Kwa hivyo, haifailii uungu wake kuwaacha bure au kuwapuuza. Na ikiwa walichopewa Manabii ni kutoka kwa Mola wao Mlezi, basi ndani yake kuna tafauti baina ya Manabii na wale wanaodai unabii. Na kwamba tofauti kati yao hutokea mara tu unapojua wanachokilingania. Mitume hawalinganii ila kwa heri, na wala hawakatazi isipokuwa kila shari. Na kila mmoja wao anamsadikisha mwenzake, na kumshuhudia haki bila ya kupingana wala kutenguana kwa sababu imetoka kwa Mola wao Mlezi. "Na lau kuwa imetoka kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu bila ya shaka wangelikuta ndani yake khitilafu nyingi." Na hii ni tofauti na wale waliodai unabii. Hakuna budi watenguane katika habari zao, amri zao, na makatazo yao, kama linavyojulikana hilo kutokana na kuzichunguza hali zao wote, kikajulikana wanachokilingania. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu alipobainisha kila kitu ambacho mtu anapaswa kukiamini kwa ujumla na kwa namna maalumu, na ikawa kauli haitoshi bila ya vitendo, akasema, "na sisi kwake tumesilimu." Yani tunaunyenyekea ukuu wake, tunatekeleza ibada zake kwa ndani yetu na kwa nje yetu, tunamkusudia yeye tu kwa ibada zetu, kwa dalili ya kutanguliza mwathiriwa ambaye ni "kwake" kabla ya mtendaji ambaye ni, "tumesilimu". Aya hii tukufu pamoja na ufupi wake na mukhtasari wake, ilijumuisha aina tatu za Tauhidi: Tauhid Rububiyya (uungu), na Tauhid Uluhiyya (Ibada) na Tauhid Al-Asmaa was-Swifaat (majina na sifa). Na ilijumuisha kuwaamini Mitume wote na Vitabu vyote. Na inajumuisha mbinu ya kutaja cha mahususi baada ya cha jumla ili kuonyesha ubora wake (yani kile mahususi). Na inajumuisha kusadiki kwa moyo, ulimi, na viungo, na kumkusudia Mwenyezi Mungu katika hayo. Na inajumuisha kutofautisha kati ya Mitume wa kweli na wenye kudai unabii miongoni mwa waongo. Na inajumuisha ufundishaji wa Muumba kwa waja wake jinsi ya kusema, na rehema zake na wema wake juu yao kwa neema za kidini ambazo zinaungana na furaha ya duniani na ya Akhera. Hivyo, ametakasika aliyekifanya Kitabu chake kuwa cha kubainisha kila kitu, na uwongofu na rehema kwa watu wanaoamini.