As-Saff
This is a translation of Tafsīr as-Saʿdī as IslamHouse.com publishes it at saadi.islamenc.com, read from that site’s pages. The site does not say who translated it or which printed edition it follows, and states no terms for taking its text, so the right to show it is not verified. Nobody has compared it with a printed book, and no scholar has reviewed it. Each passage stands beside the verses it comments on, which are the Qur’ān text of Tanzil, shown as it is there; a verse the site gives no commentary of its own stands with the passage before it, and the index names each such verse. Sabīl did not write or translate any of it.
Text fromsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)taken 2026-10-22
هُوَ ٱلَّذِىٓ أَرْسَلَ رَسُولَهُۥ بِٱلْهُدَىٰ وَدِينِ ٱلْحَقِّ لِيُظْهِرَهُۥ عَلَى ٱلدِّينِ كُلِّهِۦ وَلَوْ كَرِهَ ٱلْمُشْرِكُونَ 9
{9} Kisha akataja sababu ya kudhihiri na ushindi wa Dini ya Kiislamu, za kuonekana na zisizoonekana, akasema: “Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uwongofu na Dini ya haki” yaani: kwa elimu yenye manufaa na matendo mema. Kwa elimu yenye kuongoa kwenda kwa Mwenyezi Mungu na kwenye maskani ya utukufu wake, yenye kuongoa kufikia matendo na maadili mema zaidi, na yenye kuongoa kufikia masilahi ya dunia na Akhera, “na Dini ya haki” Yaani, Dini ambayo kwayo mtu humfuata na kumuabudu Mola Mlezi wa walimwengu wote, ambayo ni ya haki na ya ukweli, isiyo na upungufu wowote wala dosari ndani yake. Bali amri zake ni lishe ya nyoyo na nafsi, na ni raha kwa miili. Na kuacha makatazo yake ni kusalimika kutoakana na maovu na uharibifu. Kwa hivyo yale aliyotumwa nayo Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake – ya uwongofu na dini ya haki ni ushahidi mkubwa zaidi juu ya ukweli wake. Nayo ni hoja yenye kusalia maadamu zama bado zimebakia. Kila mwenye akili anavyoitafakari, anazidi kwayo furaha na ufahamu wake, “ili ipate kuzishinda dini zote” kwa hoja na ushahidi, na kuwapa ushindi watu wake wanaoisimamisha kwa upanga na mkuki. Ama dini yenyewe, haya ndiyo maelezo ambayo hayaachani nayo kila wakati, na haiwezekani kwa mshindi yeyote kuishinda au mpinzani yeyote kubishana nayo isipokuwa itampasua na kumkatisha tamaa kabisa, nayo anasalia iimedhihirika na kushinda. Na ama wanaohusiana nayo, wanapoitekeleza na wakaangaza kwa nuru yake na wakaongoka kwa uwongofu wake katika masilahi ya dini yao na maisha yao ya kidunia, hao pia hakuna atakayesimama dhidi yao, na lazima watapata ushindi dhidi ya watu wa dini zote. Lakini wakipoteza na wakaridhika na kujihusisha nayo tu, hilo haliwezi kuwanufaisha, na kuipuuza kwao huko kunakuwa sababu ya maadui kuwatawala, na hilo analijua vyema mwenye kuzichunguza hali na kuangalia katika Waislamu wa mwanzo na wa mwisho.