Skip to content
Tafsir As-Saadi - Swahili · Al-Mumtahana
Sūrah 60

Al-Mumtahana

This is a translation of Tafsīr as-Saʿdī as IslamHouse.com publishes it at saadi.islamenc.com, read from that site’s pages. The site does not say who translated it or which printed edition it follows, and states no terms for taking its text, so the right to show it is not verified. Nobody has compared it with a printed book, and no scholar has reviewed it. Each passage stands beside the verses it comments on, which are the Qur’ān text of Tanzil, shown as it is there; a verse the site gives no commentary of its own stands with the passage before it, and the index names each such verse. Sabīl did not write or translate any of it.

Text fromsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)taken 2026-10-22

Verse 10

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوٓا۟ إِذَا جَآءَكُمُ ٱلْمُؤْمِنَـٰتُ مُهَـٰجِرَٰتٍ فَٱمْتَحِنُوهُنَّ ۖ ٱللَّهُ أَعْلَمُ بِإِيمَـٰنِهِنَّ ۖ فَإِنْ عَلِمْتُمُوهُنَّ مُؤْمِنَـٰتٍ فَلَا تَرْجِعُوهُنَّ إِلَى ٱلْكُفَّارِ ۖ لَا هُنَّ حِلٌّ لَّهُمْ وَلَا هُمْ يَحِلُّونَ لَهُنَّ ۖ وَءَاتُوهُم مَّآ أَنفَقُوا۟ ۚ وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ أَن تَنكِحُوهُنَّ إِذَآ ءَاتَيْتُمُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ ۚ وَلَا تُمْسِكُوا۟ بِعِصَمِ ٱلْكَوَافِرِ وَسْـَٔلُوا۟ مَآ أَنفَقْتُمْ وَلْيَسْـَٔلُوا۟ مَآ أَنفَقُوا۟ ۚ ذَٰلِكُمْ حُكْمُ ٱللَّهِ ۖ يَحْكُمُ بَيْنَكُمْ ۚ وَٱللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ 10

{10} Ulipohitimishwa Mkataba wa Hudaybiyyah; Nabii– Rehema na Amani za Mwenyezi Mungu zimshukie – alifanya suluhu na washirikina kwa sharti kwamba yeyote miongoni mwao atakayewajia Waislamu akiwa ni Muislamu, kwamba italazimu arudishwe kwa washirikina, na hili lilikuwa neno la jumla kabisa ambalo kwa ujumla wake linajumuisha wanawake na wanaume. Ama wanaume, Mwenyezi Mungu hakumkataza Mtume wake kuwarejesha kwa makafiri kwa kutimiza sharti hilo na kukamilisha suluhu ambayo ni miongoni mwa masilahi makubwa zaidi. Ama wanawake, pindi kuwarudisha kwao kulikuwa na maovu mengi, aliwaamrisha Waumini wakijiwa na “wanawake Waumini waliohama” na wakawa na shaka kuhusu imani yao kwamba wawape mtihani kwa kitu cha kudhihirisha ukweli wao, kama vile viapo vikali na mambo mengineyo. Kwa maana, inawezekana kwamba imani yao hiyo si ya kweli, bali ni kwa kutaka tu mume, nchi, au malengo mengine ya kidunia. Kwa hivyo ikiwa wanasifika hivi, basi inalazimu warudishwe kwa washirikina katika kutimiza sharti walilowekeana na Waislamu bila ya kuleta madhara yoyote. Na ikiwa watawatia mtihanini na wakawaona kuwa ni wakweli, au wakajua hilo kwao bila ya kuwapa mtihani, basi hawakufaa kuwarudisha kwa makafiri. “Wanawake hao si halali kwa hao makafiri, wala hao makafiri hawahalalikii wanawake Waumini.” Kwa maana, huu ni uharibifu mkubwa [katika kuwarusha huko] ambao Mwenye sheria aliuzingatia na pia akazingatia utimizaji wa sharti; Kwamba wawape makafiri kile walichotumia kwa ajili ya wake zao kama vile mahari na gharama zinazohusiana nao kwa kubadilishana nao, na hapo hakuna ubaya kwa Waislamu kuwaoa, hata kama wana waume katika nchi za ushirikina lakini kwa sharti kwamba wawape ujira wao kama vile mahari na matunzo. Kama vile mwanamke wa Kiislamu si halali kwa kafiri, kadhalika, mwanamke kafiri haruhusiwi kwa mwanamume Mwislamu maadamu bado yuko katika ukafiri wake, isipokuwa Watu wa Kitabu. Ndiyo maana Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: “Wala msiwaweke wanawake makafiri katika kifungo cha ndoa zenu.” Na ikiwa ni haramu kushikilia kifungo chao cha ndoa, basi hata kukianzisha kwa kuwaoa kinafailia zaidi kukatazwa. “Na takeni mlichokitoa” enyi Waumini, watakaporudi wake zenu kwa makafiri kwa kutoka kwa Uislamu. Na ikiwa makafiri wanachukua kutoka kwa Waislamu matunzo waliyoyatoa juu ya ya wake zao waliosilimu, basi Waislamu wanastahiki pia kupata fidia kwa kile walichotoa juu ya wake zao waliokwenda kwa makafiri. Katika hili kuna ushahidi kwamba kuondoka kwa tendo la ndoa kwa mume ni kitu kinachoweza kupimwa thamani yake. Kwa hivyo, ikiwa mharibifu ataharibu ndoa ya mke wa mwanamume fulani kwa njia ya kunyonyesha au vinginevyo, basi itamlazimu adhamini mahari aliyotoa. Na kauli yake: “Hiyo ndiyo hukumu ya Mwenyezi Mungu” aliyoitaja, akaibainisha na akaiweka wazi, ni hukumu ya Mwenyezi Mungu. “Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua mno, Mwenye hekima.” Basi anazijua hukumu zinazokufaeni, kwa hivyo akaziweka katika sheria yenu kulingana na hekima yake na rehema zake.