Al-Maaida
This is a translation of Tafsīr as-Saʿdī as IslamHouse.com publishes it at saadi.islamenc.com, read from that site’s pages. The site does not say who translated it or which printed edition it follows, and states no terms for taking its text, so the right to show it is not verified. Nobody has compared it with a printed book, and no scholar has reviewed it. Each passage stands beside the verses it comments on, which are the Qur’ān text of Tanzil, shown as it is there; a verse the site gives no commentary of its own stands with the passage before it, and the index names each such verse. Sabīl did not write or translate any of it.
Text fromsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)taken 2026-10-22
وَقَالَتِ ٱلْيَهُودُ يَدُ ٱللَّهِ مَغْلُولَةٌ ۚ غُلَّتْ أَيْدِيهِمْ وَلُعِنُوا۟ بِمَا قَالُوا۟ ۘ بَلْ يَدَاهُ مَبْسُوطَتَانِ يُنفِقُ كَيْفَ يَشَآءُ ۚ وَلَيَزِيدَنَّ كَثِيرًا مِّنْهُم مَّآ أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ طُغْيَـٰنًا وَكُفْرًا ۚ وَأَلْقَيْنَا بَيْنَهُمُ ٱلْعَدَٰوَةَ وَٱلْبَغْضَآءَ إِلَىٰ يَوْمِ ٱلْقِيَـٰمَةِ ۚ كُلَّمَآ أَوْقَدُوا۟ نَارًا لِّلْحَرْبِ أَطْفَأَهَا ٱللَّهُ ۚ وَيَسْعَوْنَ فِى ٱلْأَرْضِ فَسَادًا ۚ وَٱللَّهُ لَا يُحِبُّ ٱلْمُفْسِدِينَ 64
{64} Yeye Mtukufu anajulisha kuhusu maneno ya Mayahudi mabaya, na itikadi yao mbovu, kwa hivyo Akasema, "Na Mayahudi walisema: Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba." Yaani, kuhusiana na heri, na ihsan, na wema. "Mikono yao ndiyo iliyofumba, na wamelaaniwa kwa sababu ya waliyoyasema." Na huku ni ili kuwaapiza kwa sawa na kauli yao. Kwa maana maneno yao yalijumuisha kumweleza Mwenyezi Mungu, Mkarimu kuwa ni bahili na asiyefanya wema. Kwa hivyo Akawalipa kwamba maelezo haya yanathibitika juu yao sawasawa. Basi wakawa ndio mabahili wa watu wote, na wachache wao zaidi katika wema, na wabaya wao zaidi katika kumdhania Mwenyezi Mungu. Na walio mbali wao zaidi na rehema yake ambayo ilienea kila kitu, na iliyojaa pande zote za dunia ya juu na ya chini. Na ndio maana akasema, "Bali mikono yake iko wazi. Hutoa apendavyo." Hakuna cha kumkataza wala cha kumzuia chenye kumzuia kile anachotaka. Kwani, Yeye Mtukufu alipanua fadhila yake, na wema wake wa kidini na wa kidunia, na amewaamrisha waja wake wazitafute pepo za ukarimu wake, na kwamba wasijifungie wenyewe milango ya ihsani yake kwa maasia yao. Mkono wake hutoa kwa wingi mchana na usiku, na heri yake humiminwa katika kila wakati. Huondoa dhiki, na huondoa huzuni, humtosheleza masikini, na huwakomboa mateka, na huwaunga waliovunjika, na humjibu mwenye kuomba, na humpa fakiri mwenye umaskini. Na humjibu walio katika ugumu mkubwa, na huwaitikia wanaomuomba, na anamneemesha yule ambaye hakumuomba, na humuweka salama mwenye kutafuta salama. Wala hamnyimi muasi katika heri yake, bali heri yake anachunga kwayo mwema, na muovu, na anawapa kwa wingi marafiki wake wandani kwa kuwawezesha kufanya matendo mema. Kisha anawasifu juu yake, na anawahusisha na hayo hali ya kuwa ni katika ukarimu wake, na anawalipa juu yake malipo ya sasa na ya baadaye ambayo hayawezi kuelezwa wala hayawezi kupita katika mawazo ya mja. Na anawafanyia upole katika mambo yao yote, na anawafikishia katika wema, na kuwazuia katika adhabu kiasi cha yale ambayo hawahisi mengi yake. Basi Ametakasika Yeye ambaye kila neema ambazo wanazo waja ni kutoka kwake, na kwake ndiko wanakokimbilia katika kuwazuia machukizo. Na ni Mwingi wa baraka ambaye hakuna anayeweza kumsifu vyema, bali Yeye ni kama alivyojisifu Mwenyewe. Na ametukuka Yeye ambaye waja wake hawakosi katika ukarimu wake hata kwa kiasi cha kupepesa jicho. Bali hata hakuna kuwepo kwao wala kubakia isipokuwa ukarimu wake. Mwenyezi Mungu amfedheheshe mwenye kujitosheleza kwa ujinga wake na Mola wake Mlezi, na akamnasibisha na yale yasiyostahiki utukufu wake. Bali lau Mwenyezi Mungu angeliwatendea Mayahudi waliosema kauli hiyo, na mfano wao miongoni mwa wale ambao hali yao ni sawa na hali yao katika baadhi ya kauli zao, basi wangeangamia na kupata taabu katika dunia yao. Lakini wanasema kauli hizo, naye Mtukufu anawafanyia upole, na anayaachilia hayo mbali, na anawapa muhula, wala hawapuuzi. Na kauli yake, "Kwa yakini yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Mola wako Mlezi yatawazidishia wengi katika wao uasi na kufuru." Na hii ndio adhabu kubwa zaidi kwa mja. Kwamba uwe ukumbusho ambao Mwenyezi Mungu aliteremsha kwa Mtume wake ambao ndani yake kuna uhai wa moyo na roho, na furaha ya dunia na akhera, na kufaulu kwa Nyumba mbili hizi. Ambayo ndiyo neema kubwa zaidi ambayo Mwenyezi Mungu amewaneemesha kwayo waja wake. Iliwalazimu waja kuharakisha kuukubali na kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu kwa huo, na kumshukuru Mwenyezi Mungu juu yake, kwamba uwe mfano wa huu ni kuongezeka kwa upotovu wake, na uasi juu ya uasi, na ukafiri juu ya ukafiri wake. Na hilo ni kwa sababu ya kupeana kwake mgongo hayo na kuyakataa kwake, na kuyafanyia ukaidi, na kuyapinga kwake kwa mkanganyiko batili. "Na Sisi tumewatilia uadui na chuki baina yao mpaka Siku ya Qiyama," basi hawataungana, wala hawatasaidiana, wala hawatakubaliana katika hali ambayo ina maslahi yao. Bali hawajaacha kuchukiana wao kwa wao katika nyoyo zao, wakifanyiana uadui katika vitendo vyao mpaka Siku ya Qiyama. "Kila mara wanapowasha moto wa vita" ili waufanyie Uislamu vitimbi kwa hayo na watu wake, na wakaonyesha, na wakarudia, na wakakusanya wapanda farasi na askari wa kwa miguu. "Mwenyezi Mungu anauzima" kwa kuwaangusha, na kutawanyika kwa wanajeshi wao, na ushindi wa Waislamu juu yao. "Na wanajitahidi kuleta uharibifu katika ardhi; yaani, wanafanya jitihada na bidii, lakini kwa kufanya uharibifu katika ardhi kwa kufanya maasia na kuilingania dini yao batili, na kuwazuia watu kuingia katika Uislamu. "Na Mwenyezi Mungu hawapendi waharibifu." Bali anawachukia kwa chuki kubwa, na atawalipa kwa hayo.