Al-Maaida
This is a translation of Tafsīr as-Saʿdī as IslamHouse.com publishes it at saadi.islamenc.com, read from that site’s pages. The site does not say who translated it or which printed edition it follows, and states no terms for taking its text, so the right to show it is not verified. Nobody has compared it with a printed book, and no scholar has reviewed it. Each passage stands beside the verses it comments on, which are the Qur’ān text of Tanzil, shown as it is there; a verse the site gives no commentary of its own stands with the passage before it, and the index names each such verse. Sabīl did not write or translate any of it.
Text fromsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)taken 2026-10-22
وَإِذْ أَوْحَيْتُ إِلَى ٱلْحَوَارِيِّـۧنَ أَنْ ءَامِنُوا۟ بِى وَبِرَسُولِى قَالُوٓا۟ ءَامَنَّا وَٱشْهَدْ بِأَنَّنَا مُسْلِمُونَ 111 إِذْ قَالَ ٱلْحَوَارِيُّونَ يَـٰعِيسَى ٱبْنَ مَرْيَمَ هَلْ يَسْتَطِيعُ رَبُّكَ أَن يُنَزِّلَ عَلَيْنَا مَآئِدَةً مِّنَ ٱلسَّمَآءِ ۖ قَالَ ٱتَّقُوا۟ ٱللَّهَ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ 112 قَالُوا۟ نُرِيدُ أَن نَّأْكُلَ مِنْهَا وَتَطْمَئِنَّ قُلُوبُنَا وَنَعْلَمَ أَن قَدْ صَدَقْتَنَا وَنَكُونَ عَلَيْهَا مِنَ ٱلشَّـٰهِدِينَ 113 قَالَ عِيسَى ٱبْنُ مَرْيَمَ ٱللَّهُمَّ رَبَّنَآ أَنزِلْ عَلَيْنَا مَآئِدَةً مِّنَ ٱلسَّمَآءِ تَكُونُ لَنَا عِيدًا لِّأَوَّلِنَا وَءَاخِرِنَا وَءَايَةً مِّنكَ ۖ وَٱرْزُقْنَا وَأَنتَ خَيْرُ ٱلرَّٰزِقِينَ 114 قَالَ ٱللَّهُ إِنِّى مُنَزِّلُهَا عَلَيْكُمْ ۖ فَمَن يَكْفُرْ بَعْدُ مِنكُمْ فَإِنِّىٓ أُعَذِّبُهُۥ عَذَابًا لَّآ أُعَذِّبُهُۥٓ أَحَدًا مِّنَ ٱلْعَـٰلَمِينَ 115 وَإِذْ قَالَ ٱللَّهُ يَـٰعِيسَى ٱبْنَ مَرْيَمَ ءَأَنتَ قُلْتَ لِلنَّاسِ ٱتَّخِذُونِى وَأُمِّىَ إِلَـٰهَيْنِ مِن دُونِ ٱللَّهِ ۖ قَالَ سُبْحَـٰنَكَ مَا يَكُونُ لِىٓ أَنْ أَقُولَ مَا لَيْسَ لِى بِحَقٍّ ۚ إِن كُنتُ قُلْتُهُۥ فَقَدْ عَلِمْتَهُۥ ۚ تَعْلَمُ مَا فِى نَفْسِى وَلَآ أَعْلَمُ مَا فِى نَفْسِكَ ۚ إِنَّكَ أَنتَ عَلَّـٰمُ ٱلْغُيُوبِ 116 مَا قُلْتُ لَهُمْ إِلَّا مَآ أَمَرْتَنِى بِهِۦٓ أَنِ ٱعْبُدُوا۟ ٱللَّهَ رَبِّى وَرَبَّكُمْ ۚ وَكُنتُ عَلَيْهِمْ شَهِيدًا مَّا دُمْتُ فِيهِمْ ۖ فَلَمَّا تَوَفَّيْتَنِى كُنتَ أَنتَ ٱلرَّقِيبَ عَلَيْهِمْ ۚ وَأَنتَ عَلَىٰ كُلِّ شَىْءٍ شَهِيدٌ 117 إِن تُعَذِّبْهُمْ فَإِنَّهُمْ عِبَادُكَ ۖ وَإِن تَغْفِرْ لَهُمْ فَإِنَّكَ أَنتَ ٱلْعَزِيزُ ٱلْحَكِيمُ 118 قَالَ ٱللَّهُ هَـٰذَا يَوْمُ يَنفَعُ ٱلصَّـٰدِقِينَ صِدْقُهُمْ ۚ لَهُمْ جَنَّـٰتٌ تَجْرِى مِن تَحْتِهَا ٱلْأَنْهَـٰرُ خَـٰلِدِينَ فِيهَآ أَبَدًا ۚ رَّضِىَ ٱللَّهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا۟ عَنْهُ ۚ ذَٰلِكَ ٱلْفَوْزُ ٱلْعَظِيمُ 119 لِلَّهِ مُلْكُ ٱلسَّمَـٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضِ وَمَا فِيهِنَّ ۚ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَىْءٍ قَدِيرٌۢ 120
{111 - 120} Yaani, na kumbuka neema yangu juu yako nilipokurahisishia wafuasi na wasaidizi, basi nikawafunulia wahyi wanafunzi, na nikatia kuniamini Mimi na Mtume wangu katika nyoyo zao, au niliwafunulia wahyi kwa ulimi wako. Yaani, niliwaamrisha kwa wahyi ambao ulikujia kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa hivyo wakaitikia hilo na wakafuata, na wakasema, "Tumeamini, na shuhudia kuwa sisi hakika ni Waislamu." Wakajumuisha kati ya Uislamu wa nje na kufuata kwa matendo mema na imani ya ndani ambayo, unamtoa mwenyewe kutoka unafiki na kutoka katika udhaifu wa imani. Na Al-hawariyyun ni wale wanaonusuru. Kama Mwenyezi Mungu Mtukufu alivyosema; kama vile Isa bin Maryam alivyowaambia wanafunzi wake, “Ni nani wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu? Wanafunzi Wakasema: Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu!” "Wanafunzi waliposema: Ewe Isa bin Maryamu! Je, Mola wako Mlezi anaweza kututeremshia meza yenye chakula kutoka mbinguni?" Yaani, meza yenye chakula juu yake. Na hili si kutokana na shaka yao juu ya nguvu za Mwenyezi Mungu na uwezo wake juu ya hilo. Bali ni katika njia ya kuwasilisha ombi na adabu nzuri kutoka kwao. Na kwa kuwa kuomba Aya za mapendekezo ni kinyume na kufuata haki, na yakawa maneno haya yaliyotoka kwa wanafunzi huenda yanaweza kuleta fikira hiyo potofu, Isa amani iwe juu yake akawaaidhi na kusema: "Mcheni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni Waumini." Kwa maana, Muumini anabebwa na imani aliyo nayo kushikamana na uchamungu, na kufuata amri ya Mwenyezi Mungu, na wala haombi katika aya anazopendekeza yeye ambazo baada yake hajui kitakachotokea. Basi Wanafunzi wakajulisha kwamba makusudio yao hayakuwa na maana hii, bali wana makusudio mema na kwa ajili ya haja juu ya hilo. Wakasema; "Tunataka kula kwayo," na huu ni ushahidi ya kwamba walikuwa wanakihitaji. "Na nyoyo zetu zitue" kwa imani wakati tunapoziona Aya kwa macho, ili imani yetu iwe yakini ya jicho. [Kama ilivyokuwa elimu ya yakini kabla ya hapo], Kama Al-Khalil (Ibrahim), amani iwe juu yake, alivyomwomba Mola wake Mlezi amwonyeshe jinsi anavyowahuisha wafu. "Mwenyezi Mungu akasema: Kwani huamini? Akasema: Hasha! Lakini ili moyo wangu utue." Basi mja anahitaji kuongeza elimu, na yakini, na imani kila wakati. Na ndiyo maana akasema, “Na tujue kwamba umetuambia ukweli. Yaani, tujue ukweli wa yale uliyokuja nayo kwamba ni haki na ukweli, "na tuwe miongoni mwa wanaoshuhudia juu ya hilo." Kwa hivyo liwafae wale walio baada yetu, na sisi tuwe mashahidi wako kwa hilo, kwa hivyo hoja iwe imesimama, na uthibitisho uongezeke kwa hilo. Isa, amani na baraka ziwe juu yake, aliposikia hayo, na akajua makusudio yao, akawaitikia ombi lao kwa hivyo akasema:”Ewe Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wetu! Tuteremshie meza yenye chakula kutoka mbinguni ili kiwe kwetu Sikukuu, kwa ajili ya wa mwanzo wetu na wa mwisho wetu, na kiwe ni Ishara itokayo kwako. Yaani, uwe wakati wa kuteremka kwake ni sikukuu na msimu ambao Aya hii kubwa itakumbukwa, kwa hivyo ihifadhiwe na wala isisahaulike pamoja na kupita kwa wakati na kurudiarudia kwa miaka. Kama vile Mwenyezi Mungu Mtukufu alivyozifanya sikukuu za Waislamu kuwa ni ukumbusho wa Aya zake, na tanabahisho juu ya Sunna za Mitume na njia zao zilizonyooka sawasawa; na fadhila zake, na wema wake kwao. "Basi turuzuku, kwani Wewe ndiwe mbora zaidi wa wanaoruzuku;" yaani, uifanye kuwa ni riziki kwetu. Basi Isa amani iwe juu yake, akaomba kuteremka kwake na kwamba iwe kwa masilahi haya mawili: masilahi ya dini, ambayo ni kwamba iwe ushahidi wa kubakia, na maslahi ya dunia, ambayo ni kwamba iwe riziki. "Mwenyezi Mungu akasema: Hakika Mimi nitawateremshia hicho. Lakini yeyote katika nyinyi atakayekufuru baadaye, basi hakika Mimi nitamuadhibu adhabu nisiyomuadhibu yeyote katika walimwengu." Kwa sababu alishuhudia Ishara ya kushangaza lakini akakufuru kutokana na ukaidi na dhuluma, kwa hivyo akastahiki adhabu chungu na mateso makali. Na jua ya kwamba, Mwenyezi Mungu Mtukufu aliahidi kuwa ataiteremsha, na akawaahidi adhabu iwapo wataikufuru ahadi hii, na wala hakutaja kuwa aliiteremsha; kwa hivyo inawezekana kwamba hakuiteremsha kwa sababu hawakuchagua kufanya hivyo. Na hilo linaonyeshwa na ukweli kwamba halikutajwa katika Injili ambayo iko mikononi mwa Wakristo na haipo popote pale. Na inawezekana kwamba aliiteremsha kama alivyoahidi Mwenyezi Mungu, na kwamba havunji ahadi yake, na inakuwa kwamba kutotajwa kwake katika Injili zilizomo mikononi mwao ni katika fungu ambalo walikumbushwa kwalo na wakalisahau, au kwamba halikutajwa kabisa katika Injili. Bali hilo lilikuwa likirithiwa miongoni mwao, likipitishwa na waliokuja kutoka kwa watangulizi wao, kwa hivyo mwenyezi Mungu akatosheka na hilo kwa kutolitaja katika Injili. Na maana hii inaonyeshwa na kauli yake, "na tuwe miongoni mwa wanaoshuhudia juu ya hilo." Na Mwenyezi Mungu ndiye anayejua zaidi uhakika wa hali hiyo. "Na pale Mwenyezi Mungu aliposema: Ewe Isa bin Maryam! Je, wewe ndiye uliwaambia watu: Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni miungu wawili badala ya Mwenyezi Mungu? " Na hili ni karipio kwa Wakristo waliosema kuwa: Hakika Mwenyezi Mungu ni wa tatu wa watatu! Kwa hivyo mwenyezi Mungu atamwambia Isa maneno haya, naye Isa atajitenga nayo. Na atasema, "Subhanaka (Wewe umetakasika!)" kutokana na maneno haya mabaya, na kutokana na yasiyokufaa, "Hainifailii mimi kusema ambayo si haki yangu"; yaani, sipaswi, na haifai niseme chochote ambacho si katika sifa zangu wala katika haki zangu. Kwani hakuna hata mmoja katika viumbe, wala malaika wa walio karibu na Mwenyezi Mungu, wala Manabii waliotumwa, wala mtu mwingine yeyote, mwenye haki wala anayestahiki hadhi ya uungu. Bali, wote ni waja, wanaendeshwa, na ni viumbe waliotiishwa, na masikini, wasiojiweza. "Ikiwa nilisema, basi bila ya shaka umekwisha yajua. Wewe unayajua yaliyo ndani ya nafsi yangu, lakini mimi siyajui yaliyo katika nafsi yako." Basi Wewe ndiwe unayejua zaidi yale yaliyotoka kwangu, na wewe ndiwe Mjuzi wa ghaibu. Na haya ni katika utimilifu wa adabu ya Masihi , rehema na amani ziwe juu yake, katika kuzungumza na Mola wake Mlezi. Yeye, amani iwe juu yake, hakusema: Mimi sikusema lolote katika hayo. Bali aliseama maneno ambayo anajikania nafsi yake, kwamba alisema kila maneno yanayopingana na nafasi yake ya utukufu, na kwamba hili ni miongoni mwa mambo yasiyowezekana. Na akamtakasa Mola wake Mlezi kutokana na hilo kwa utakaso mkamilifu zaidi, na akarudisha elimu kwa Mwenye kujua ghaibu na yenye kushuhudiwa. Kisha akataja waziwazi aliyowaamrisha Wana wa Israili, kwa hivyo akasema, "Sikuwaambia lolote isipokuwa yale uliyoniamrisha; "kwani mimi ni mja ninayefuata amri yako wala siufanyii ujasiri utukufu wako. "Kwamba, muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi. Yaani,sikuwaamrisha isipokuwa kumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake, na kumfanyia Yeye tu Dini ambalo linajumuisha kukataza kunifanya mimi na mama yangu kuwa waungu wawili kando na Mwenyezi Mungu, na kubainisha kuwa mimi ni mja ninyelelewa. Kwa hivyo, kama vile Yeye ni Mola wenu Mlezi, Yeye pia ndiye Mola wangu Mlezi, "Na mimi nilikuwa shahidi juu yao nilipokuwa miongoni mwao." Ninamshuhudia yule aliyefanya jambo hili na yule ambaye hakulifanya. "Na uliponifisha, ukawa Wewe ndiwe Muangalizi juu yao;" yaani, mwenye kujua siri zao na dhamiri zao, "Na Wewe ni shahidi juu ya kila kitu;" kwa elimu, na kusikia, na kuona. Kwa maana elimu yako imezizunguka habari zote, na kusikia kwako kumezunguka yanayosikika, na kuona kwako kumezunguka yanayoonekana. Basi Wewe ndiye utakayewalipa waja wako kwa yale unayoyajua ndani yao ya heri na maovu. "Ukiwaadhibu, basi hao ni waja wako." Nawe unawarehemu zaidi kuliko wao wenyewe kwa nafsi zao, na unazijua zaidi hali zao. Na lau kuwa wao si waja waasi, basi hungewaadhibu. "Na ukiwafutia dhambi, basi Wewe ndiwe Mwenye nguvu." Yaani, kufuta kwako dhambi kunatokana na nguvu kamili, na uwezo kamili, si kama mwenye kufuta dhambi kwa sababu ya kushindwa kwake na kutoweza. "Mwenye hekima," kwani ilikuwa ni katika matakwa ya hekima yako kwamba umfutie dhambi mwenye kufanya sababu za kufutiwa dhambi. "Mwenyezi Mungu akasema," akiibainisha hali ya waja wake Siku ya Qiyama, na ni nani kati yao atafaulu, na ni nani ataangamia, na ni nani mwenye taabu, na ni nani mwenye furaha. "Hii ndiyo Siku ambayo wasemao ukweli utawafaa ukweli wao. Na wakweli ni wale ambao vitendo vyao, na maneno yao, na makusudio yao yalinyooka kwenye njia iliyonyooka na uwongofu ulio sawasawa. Basi Siku ya Kiyama, watapata matunda ya ukweli huo wakati mwenyezi Mungu atawaweka katika makalio ya kweli kwa Mfalme Mwenye uweza. Ndiyo maana Akasema, "Wao wana Mabustani yapitayo mito chini yake. Humo watadumu milele. Mwenyezi Mungu amewawia radhi, nao walimridhia. Huku ndiko kufuzu kukubwa." Nao waongo kinyume nao watapata madhara ya uongo wao na kuzua kwao, na matunda ya matendo yao maovu. "Ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi" kwa sababu Yeye ndiye Muumba wake na ndiye Mwenye kuendesha mambo kwa hukumu yake ya kimajaaliwa, na hukumu yake ya kisheria, na hukumu yake ya kimalipo. Na ndiyo maana akasema, "Naye ni Muweza wa kila kitu." Basi hakuna linaloweza kumshinda, bali vitu vyote vinafuata mapenzi yake, vimewekwa chini ya amri yake.
Imetimia Tafsir ya Surah Al-Ma'idah kwa fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wema wake. Na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote.