Skip to content
Tafsir As-Saadi - Swahili · An-Nisaa
Sūrah 4

An-Nisaa

This is a translation of Tafsīr as-Saʿdī as IslamHouse.com publishes it at saadi.islamenc.com, read from that site’s pages. The site does not say who translated it or which printed edition it follows, and states no terms for taking its text, so the right to show it is not verified. Nobody has compared it with a printed book, and no scholar has reviewed it. Each passage stands beside the verses it comments on, which are the Qur’ān text of Tanzil, shown as it is there; a verse the site gives no commentary of its own stands with the passage before it, and the index names each such verse. Sabīl did not write or translate any of it.

Text fromsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)taken 2026-10-22

Verse 34

ٱلرِّجَالُ قَوَّٰمُونَ عَلَى ٱلنِّسَآءِ بِمَا فَضَّلَ ٱللَّهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَآ أَنفَقُوا۟ مِنْ أَمْوَٰلِهِمْ ۚ فَٱلصَّـٰلِحَـٰتُ قَـٰنِتَـٰتٌ حَـٰفِظَـٰتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ ٱللَّهُ ۚ وَٱلَّـٰتِى تَخَافُونَ نُشُوزَهُنَّ فَعِظُوهُنَّ وَٱهْجُرُوهُنَّ فِى ٱلْمَضَاجِعِ وَٱضْرِبُوهُنَّ ۖ فَإِنْ أَطَعْنَكُمْ فَلَا تَبْغُوا۟ عَلَيْهِنَّ سَبِيلًا ۗ إِنَّ ٱللَّهَ كَانَ عَلِيًّا كَبِيرًا 34

{34} Yeye Mtukufu anajulisha kwamba “Wanaume ni wasimamizi imara wa wanawake.” Yani, wao ni wasimamizi wao kwa kuwawajibishia haki za Mwenyezi Mungu Mtukufu kama vile kuzihifadhi faradhi zake, na kuwazuia uharibifu. Nao wanaume ni juu yao kuwalazimisha kufanya hivyo. Na kuwasimamia kwao pia ni kwa kuwapa matumizi, na kuwavisha, na kuwapa makazi. Kisha akataja sababu yenye kulazimu wanaume kuwa wasimamizi juu ya wanawake, akasema; “kwa yale aliyowafadhilisha kwayo Mwenyezi Mungu baadhi yao juu ya baadhi, na kwa yale wanayoyatoa katika mali zao.” Yani kwa sababu ya ubora wa wanaume juu ya wanawake na kujiboresha kwao juu yao. Na ubora wa wanaume juu ya wanawake ni katika njia nyingi: kutokana na kwamba mamlaka ni mahususi kwa wanaume, na unabii, na utume, na kuteuliwa kwao kwa ajili ya ibada nyingi kama vile Jihadi, na swala ya Idi na swala ya Ijumaa, na kwa kile alichowawapa Mwenyezi Mungu wao hasa kama vile akili, na fikra iliyokomaa, na subira, na stahamala ambayo wanawake hawana mfano wake. Na vile vile aliwaamrisha wao tu kutoa matumizi ya wake zao. Bali na hata nyingi ya matumizi ni mahsusi tu kwa wanaume, na wanatofautiana na wanawake. Na pengine hii ndiyo siri ya kauli yake, “kwa yale wanayoyatoa” na akafuta njia zinazotolewa ili hilo lionyeshe ujumla wa kutoa, kwa hivyo ikajulikana kutokana na haya yote kwamba mwanamume ni kama mlezi na bwana kwa mke wake. Naye, kwake ni mtumwa, mfungwa, na mtumishi. Kwa hivyo, kazi yake mwanamume ni kufanya kile ambacho Mwenyezi Mungu alimpa kulinda, na kazi yake mwanamke ni kumtii Mola wake Mlezi na kumtii mumewe. Ndio maana akasema, “Basi wanawake wema ni wale wenye kutii,” yani mtiifu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, “na wanaojilinda hata katika siri.” Yani wanaowatii waume zao hata wakiwa hawapo. Anamlinda mumewe kwa nafsi yake mwenyewe na mali yake (mumewe). Na hilo ni kwa ulinzi wa Mwenyezi Mungu kwao na kuwawezesha kwake, si kutokana nao wenyewe; kwa kuwa nafsi inaamrisha maovu. Lakini mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu, atamtosheleza kinachomtia wasiwasi katika mambo yake ya kidini na ya kidunia. Kisha akasema, “Na wale mnaochelea kutoka kwao katika utiifu.” Yani kujiinua kwao juu ya utiifu kwa waume zao, kwa kumuasi kwa maneno au kwa matendo; basi atamtia adabu kwa njia rahisi zaidi, kisha rahisi zaidi. “Basi waaidhini” Yani kwa kubainisha hukumu ya Mwenyezi Mungu katika kumtii mume na kutomuasi, na kutia moyo wa kutii, na kutishia dhidi ya kuasi. Kwa hivyo, akikomeka, basi hilo ndilo linalotakiwa, vinginevyo mume amhame katika malazi na namna kwamba halali naye wala hamjaamii kwa kiwango ambacho lengo litapatikana. Vinginevyo, ampige kipigo kisichoumiza. Ikiwa makusudio yatafikiwa kwa mojawapo ya mambo haya na wakawatii, “msitafute njia yoyote dhidi yao.” Yani mmeshapata kile mnachopenda, kwa hivyo acheni kumlaumu kwa mambo yaliyopita, na kupekua makosa ambayo yanadhuru kuyataja, na mabaya yanatokea kwa sababu yake. “Hakika, Mwenyezi Mungu ndiye aliye juu, Mkubwa.” Yani ana sifa ya kuwa juu kamili kwa namna zote na mazingatio yote. Ujuu wa dhati, na ujuu wa hadhi, na ujuu ushindi. Mkubwa ni yule ambaye hakuna mkubwa zaidi yake, wala Mtukufu wala Mkuu. Ni Mkubwa wa dhati na sifa zake.