Skip to content
Tafsir As-Saadi - Swahili · An-Nisaa
Sūrah 4

An-Nisaa

This is a translation of Tafsīr as-Saʿdī as IslamHouse.com publishes it at saadi.islamenc.com, read from that site’s pages. The site does not say who translated it or which printed edition it follows, and states no terms for taking its text, so the right to show it is not verified. Nobody has compared it with a printed book, and no scholar has reviewed it. Each passage stands beside the verses it comments on, which are the Qur’ān text of Tanzil, shown as it is there; a verse the site gives no commentary of its own stands with the passage before it, and the index names each such verse. Sabīl did not write or translate any of it.

Text fromsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)taken 2026-10-22

Verse 12

وَلَكُمْ نِصْفُ مَا تَرَكَ أَزْوَٰجُكُمْ إِن لَّمْ يَكُن لَّهُنَّ وَلَدٌ ۚ فَإِن كَانَ لَهُنَّ وَلَدٌ فَلَكُمُ ٱلرُّبُعُ مِمَّا تَرَكْنَ ۚ مِنۢ بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصِينَ بِهَآ أَوْ دَيْنٍ ۚ وَلَهُنَّ ٱلرُّبُعُ مِمَّا تَرَكْتُمْ إِن لَّمْ يَكُن لَّكُمْ وَلَدٌ ۚ فَإِن كَانَ لَكُمْ وَلَدٌ فَلَهُنَّ ٱلثُّمُنُ مِمَّا تَرَكْتُم ۚ مِّنۢ بَعْدِ وَصِيَّةٍ تُوصُونَ بِهَآ أَوْ دَيْنٍ ۗ وَإِن كَانَ رَجُلٌ يُورَثُ كَلَـٰلَةً أَوِ ٱمْرَأَةٌ وَلَهُۥٓ أَخٌ أَوْ أُخْتٌ فَلِكُلِّ وَٰحِدٍ مِّنْهُمَا ٱلسُّدُسُ ۚ فَإِن كَانُوٓا۟ أَكْثَرَ مِن ذَٰلِكَ فَهُمْ شُرَكَآءُ فِى ٱلثُّلُثِ ۚ مِنۢ بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصَىٰ بِهَآ أَوْ دَيْنٍ غَيْرَ مُضَآرٍّ ۚ وَصِيَّةً مِّنَ ٱللَّهِ ۗ وَٱللَّهُ عَلِيمٌ حَلِيمٌ 12

{12} Kisha Yeye Mtukufu akasema, "Nanyi mna," enyi waume, "nusu ya walichoacha wake zenu ikiwa hawana mtoto. Lakini ikiwa wana mtoto, basi mna robo katika kile walichokiacha, baada ya wasia waliyousia au kulipa deni. Na wake zenu wana robo katika kile mlichokiacha, ikiwa hamna mtoto. Lakini ikiwa mna mtoto, basi wana thumuni katika kile mlichokiacha, baada ya wasia mliyousia au kulipa deni." Na anaingia katika jina 'mtoto' ambaye ni sharti kuwepo kwake au kutokuwepo kwake mtoto wa kutoka katika kiuno, au mtoto mwana wa kiume, wa kiume na wa kike, mmoja na wengi, ambaye anatokana na ndoa au asiyekuwa yeye. Na anatoka katika hilo mtoto wa wasichana kwa kauli moja. Kisha Yeye Mtukufu akasema, “Na ikiwa mwanamume au mwanamke anayerithiwa ni Kalala (hana mtoto wala wazazi), lakini anaye kaka au dada,” yani wa kwa mama, kama ilivyo katika baadhi ya visomo. Na wanavyuoni wamekubaliana kwamba kinachomaanishwa na ndugu hapa ni ndugu wa kwa mama. Basi ikiwa anarithiwa Kalaala, yani maiti hana mzazi wala mwana. Yani hana baba, wala babu, wala mwana wa kiume, wala wana wa kiume wa mwana wa kiume, wala binti, wala binti ya mwana wa kiume hata wakishuka vipi. Na hii ndiyo maana ya Kalaala, kama alivyoifasiri hivyo Abu Bakr As-Siddiq, Mwenyezi Mungu amwiye radhi. Na kuna itifaki juu ya hilo, na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu. “Basi kila mmoja wao” yani, kaka na dada “ana sudusi.'' Na wakiwa zaidi kuliko hivyo,” yani, zaidi ya mmoja; “basi watashirikiana katika theluthi.” Yani, hawazidish juu ya theluthi moja hata wakiwa zaidi ya wawili. Na kauli yake, “basi watashirikiana katika theluthi” iliashiria kwamba wale wa kiume wao na wa kike wao wanalingana. Kwa sababu, neno ‘mshirika’ linalazimu kuwepo usawa. Na neno ‘Kalaala’ liliashiria kwamba dhuria hata kama watateremka vipi, na wazazi wa kiume, hata wakipanda juu vipi wanawaangusha watoto wa kwa mama. Kwa sababu, Mwenyezi Mungu hakuwarithisha isipokuwa katika hali ya Kalaala. Na ikiwa Kalaala hangekuwa anarithiwa, basi hawangerithi kitu kutoka kwake. Na kauli yake, “basi watashirikiana katika theluthi” iliashiria kwamba ndugu wa kwa baba na mama huanguka katika suala linaloitwa ‘punda’. Nalo ni wakati warithi ni mume, na mama, na ndugu wa kwa mama, na ndugu wa kwa baba na mama. Hapo, mume anapata nusu, naye mama anapata sudusi, nao ndugu wa kwa mama wanapata theluthi moja, na ndugu wa kwa mama na baba wanaanguka. Kwa sababu, Mwenyezi Mungu aliwapa theluthi ndugu wa kwa mama tu. Na ikiwa ndugu wa kwa baba na mama watawashiriki, basi hilo litakuwa kukusanya kati ya kile ambacho Mwenyezi Mungu alitenganisha hukumu yake. Na pia, kwa sababu ndugu wa kwa mama wana fungu maalum, nao ndugu wa kwa baba na mama huchukua kilichosalia. Na Nabii – rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake – alisema, “Wapeni wastahiki wa mafungu ya urithi mafungu yao. Na chochote chenye kusalia basi hicho ni cha mtu wa kiume anayestahiki zaidi.” Na watu mafungu maalumu ni wale ambao Mwenyezi Mungu aliwakadiria mafungu yao. Na katika suala hili, hakuna kitu chochote kinachobaki baada yao (watu wa mafungu), kwa hivyo wanaanguka ndugu wa kwa baba na mama. Na hili ndilo la sahihi katika suala hilo. Ama urithi wa kaka na dada wa kwa baba na mama, au wa kwa baba, basi hilo limetajwa katika kauli yake, "Wanakuomba uhukumu, sema: Mwenyezi Mungu anawapa hukumu juu ya Al-Kalaala (mtu aisiyekuwa na wana wala wazazi);" hadi mwisho wa Aya. Basi dada mmoja wa kwa baba na mama, au wa kwa baba ana nusu, nao wawili wana theluthi mbili. Naye dada mmoja wa kwa baba na mama pamoja na dada wa kwa baba au madada anachukua nusu, na kinachosalia katika zile theluthi mbili ni cha dada au dada au mama wa kwa baba, nacho ni sudusi, ili kukamilisha zile theluthi mbili (wanazostahiki wanawake). Na ikiwa madada wa kwa baba watachukua theluthi mbili zote, basi madada wa kwa baba wanaanguka, kama ilivyotangulia katika mabinti za mwana wa kiume. Na ikiwa ndugu ni wanaume na wanawake, basi wa kiume atapata mfano wa fungu la wa kike wawili. Na basi ikisemwa: Je, inapatikana katika Qur-ani au la? Hukumu ya urithi wa muuaji, na mtumwa, na yule aliye katika dini nyingine, na mtumwa nusu, na mwenye jinsia mbili, na babu akiwa pamoja na ndugu wasiokuwa wa kwa mama, na 'Awl (kuzidisha kiwango cha urithi na kupunguza mafungu), na Radd (kuwaregeshea mali kwa mara ya pili wale wanaorithi), na jamaa, na 'Aswaba (wanaochukua mali iliyosalia) wengineo, na madada wa kwa asiyekuwa mama wakiwa pamoja na wasio na mabinti au mabinti wa mwana wa kiume? Itasemwa: Ndio, ina tanabahisho na maashirio ya ndani ambazo ni vigumu kuyaelewa kwa asiyetafakari, yenye kuonyesha yote yaliyotajwa. Ama muuaji na yule ambaye ana dini tofauti, basi inajulikana kuwa wao si warithi kutokana na kubainisha hekima ya Mwenyezi Mungu, katika kuwagawia warithi mali kulingana na ukaribu wao na manufaa yao ya kidini na kidunia. Naye Mtukufu aliashiria hekima hii kwa kauli yake, "Nyinyi hamjui ni nani baina yao aliyekaribia zaidi kwenu kwa manufaa." Na ilijulikana kuwa muuaji alimfanyia mrithiwa wake madhara makubwa zaidi, kwa hivyo yale yaliyo ndani yake ya kumsababishia kurithi hayainuki kupingana na madhara ya kuua ambayo ni kinyume cha manufaa ambayo ndiyo sababu za urithi. Kwa hivyo ikajulikana kutokana na hilo kwamba kuua ndiko kizuizi kikubwa mno kinachozuia kurithi, na kinakata uhusiano wa kinasaba ambao Mwenyezi Mungu alisema kuuhusu. "Na jamaa ni karibu wao kwa wao katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu," pamoja na kwamba kanuni ya kisheria ilishatulia kwamba: yeyote anayeharakisha kitu kabla ya wakati wake, anaadhibiwa kwa kunyimwa kitu hicho. Na kwa hili na mfano wake, inajulikana kuwa mwenye kuhalifiana na dini ya mrithiwa wake, hana urithi. Na hiyo ni kwa kuwa, kimeshapingana chenye kusababisha, ambacho ni kuunga kwa nasaba ambako kunasababisha urithi, na kizuizi ambacho ni kuhalifiana katika dini ambako kunasababisha kutofautiana katika kila namna; kwa hivyo kizuizi kikawa na nguvu, na kikazuia sababu ya urithi ambayo ni nasaba. Kwa hivyo, sababu haikufanya kazi kwa sababu ya kusimama kwa kizuizi. Hili linabainisha kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amezifanya haki za Waislamu kuwa muhimu zaidi kuliko haki za kidunia za jamaa makafiri. Basi, akifa Muislamu, mali yake inahamia kwa yule ambaye anafaa zaidi na anayeistahiki zaidi. Kwa hivyo, inakuwa kauli yake Yeye Mtukufu, "Na ni jamaa wa karibu wanaostahikiana wao kwa wao katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu," ikiwa dini zao zinaafikiana. Na ama pamoja na kutofautiana kwake, undugu wa kidini unatangulizwa mbele ya undugu wa kinasaba tu. Ibn Al-Qayyim alisema katika “Jalaa Al-Afham,” “Na tafakari maana hii katika Aya ya mirathi na kufungamanisha kwa Yeye Mtakatifu kurithiana ndani yake kwa neno 'mke' badala ya 'mwanamke.' Kama katika kauli yake Yeye Mtukufu, "Nanyi mna nusu ya walichoacha wake zenu." Ni dalili ya kwamba mirathi hii imetokea kwa sababu ya ndoa tu ambayo inalazimu kufanana na uwiano. Naye Muumini na kafiri hawana mfanano wala uwiano. Kwa hivyo, haitokei baina yao kurithiana. Na siri za misamiati na muundo wa kuunganisha kwa maneno yake yako juu ya akili za walimwengu." Mwisho. Na ama mtumwa, yeye harithi wala harithiwi. Ama kutorithisha kwake, hilo liko wazi. Kwa sababu, hana mali yenye kurithiwa kutoka kwake. Bali, kila kitu alicho nacho ni cha bwana wake. Na ama kutorithi kwake, hilo ni kwa sababu hamiliki. Kwani, lau kuwa atamiliki, basi itakuwa ni ya bwana wake, naye ni hana uhusiano wa kinasaba na maiti. Kwa hivyo, inakuwa kama kauli yake Yeye aliyetukuka, "Fungu la mwanamume ni kama fungu la wanawake wawili." Na, "Nanyi mna nusu ya walichoacha wake zenu." Na "basi kila mmoja wao ana sudusi;" na mfano wake kwa yule ambaye anaweza kumiliki. Na ama mtumwa, yeye hawezi hilo, kwa hivyo ikajulikana kwamba hana urithi. Na ama yule ambaye baadhi yake ni huru na baadhi yake ni mtumwa; basi huyo hukumu zake pia inakuwa kibaadhi baadhi. Kwa hivyo, kile cha uhuru alicho nacho, yeye anastahili kwacho kile ambacho Mwenyezi Mungu alipanga katika urithi. Kwa sababu ule uhuru ulio ndani yake unamwezesha kumiliki, na utumwa ulio ndani yake haumuwezeshi hilo. Kwa hivyo, ikiwa yeye ni huru baadhi yake na ni mtumwa baadhi yake, basi anarithi na anarithiwa, na anazuia (wengine) kwa kiwango cha uhuru ulio ndani yake. Na ikiwa ni mtumwa, yeye anakuwa ni mwenye kusifiwa na kulaumiwa, analipwa thawabu na anaadhibiwa kwa kiwango cha kile kilicho ndani yake chenye kusababisha hilo. Basi huyu pia ni hivyo. Na ama mwenye jinsia mbili, basi yeye hakosi kuwa ima ana uume ulio wazi au uke, au ni ambaye hakuna kilicho wazi katika mawili hayo. Kwa hivyo, akiwa yu wazi, basi jambo lake ni wazi: ikiwa ni wa kiume, basi ana hukumu za wanaume, na maandishi yaliyojukuja kuwahusu yanamjumuisha. Na kama ni wa kike, basi ana hukumu za wanawake, na anajumuishwa na maandiko yaliyokuja kuhusiana nao. Na ikiwa amechanganya mawili hayo, na ikawa kwamba hali ya uume na hali ya uke hazitofautiani katika kiwango cha urithi, kama vile ndugu za wa kwa mama, basi hapo jambo ni wazi. Na ikiwa kurithi kwake kunatofautiana kwa kuzingatia uume wake na uke wake na tusibaki na njia ya kujua hilo, hatutampa kubwa zaidi ya makadirio mawili hayo kwa sababu ya uwezekano wa kuwadhulumu wale walio pamoja naye miongoni mwa warithi. Na hatuwezi kumpa kilicho kidogo kwa sababu ya uwezekano wa sisi kumdhulumu. Basi ikawa ni lazima kuwa katikati ya mambo mawili hayo, na kufuata ya uadilifu zaidi kati ya njia mbili hizo. Yeye Mtukufu alisema, "Fanyeni uadilifu. Hivyo ndiyo kuwa karibu mno na uchamungu." Na hatuna njia ya kuelekea kwenye uadilifu katika mfano wa hili zaidi ya njia hii iliyotangulia, na Mwenyezi Mungu haiamrishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kiwango cha iwezavyo. Basi mcheni Mwenyezi Mungu kama mwezavyo. Na ama urithi wa babu pamoja na ndugu wa kwa baba na mama, au wa kwa baba, na je wanarithi pamoja naye au hapana? Kitabu cha Mwenyezi Mungu kilionyesha maneno ya Abu Bakr As-Siddiq, Mwenyezi Mungu amwiye radhi, na kwamba babu huwazuia ndugu wa kwa baba na mama, au wa kwa baba tu, au wa kwa mama kama vile baba huwazuia. Na ubainisho wa hayo ni kwamba babu ni baba katika sehemu zaidi ya moja katika Qur-ani. Kama kauli yake Yeye Mtukufu, "yalipomfikia Yaaqub mauti, akawaambia wanawe: Mtamuabudu nani baada yangu? Wakasema: Tutamuabudu Mungu wako na Mungu wa baba zako, Ibrahim na Ismail na Is-haq..." hadi mwisho wa Aya. Naye Yusuf amani iwe juu yake alisema, "Na nimefuata mila ya baba zangu, Ibrahim, na Is-haq, na Yaa'qub." Basi Mwenyezi Mungu akamwita baba, babu na babu ya baba. Basi hilo likaashiria kuwa babu yuko katika nafasi ya baba, anarithi kile anachorithi baba, na anamzuia yule anayemzuia. Na ikiwa wanachuoni walikubaliana kwamba babu hukumu yake ni hukumu ya baba anapokosekana katika urithi wake pamoja na watoto na wengineo miongoni mwa ndugu, na akina ami na watoto wao wa kiume, na hukumu nyingine zote za urithi, basi inafaa pia hukumu yake (babu) iwe ni hukumu yake (baba) katika kuwazuia ndugu wasiokuwa wa kwa mama. Na ikiwa mwana wa kiume wa mwana wa kiume yuko katika nafasi ya mwana wa kiume wa kutoka katika kiuno, basi kwa nini asiwe babu katika nafasi ya baba? Na ikiwa babu ya baba akiwa pamoja na mwana wa kiume wa kaka wanachuoni walikubaliana kuwa anamzuia, basi kwa nini babu ya aliyekufa asimzuie kaka yake? Na hakuna maandishi yoyote, wala ishara, wala tanabahisho, wala mlinganisho sahihi kwa yule anayewarithisha ndugu wakiwa pamoja na babu. Ama masuala ya 'Awl (kuongezeka kiwango cha mali ya urithi na kipungua mafungu ya urithi) hukumu yake inatokana na Qur-ani. Na hilo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwawekea na akawakadiria watu wa urithi mafungu yao, na wapo baina ya hali mbili: ima wazuiane wao kwa wao, au hapana. Basi ikiwa watazuiana wao kwa wao, basi yule aliyezuiwa anaanguka na hasongamanishi wengine wala hastahili chochote. Na ikiwa hawazuiliani wao kwa wao, basi hali hazitoki nje ya hali kuwa mafungu hayamalizi urithi wote, au yaumalize bila ya ziada wala upungufu, au mafungu yazidi mali ya urithi. Basi katika zile hali mbili za kwanza, kila mmoja anachukua fungu lake kamili. Na katika hali ya mwisho, ambayo ni ikiwa mafungu yatazidi mali ya urithi. Na hilo halitoki nje ya hali mbili: Ima tuwapunguzie baadhi ya warithi katika fungu lake ambalo Mwenyezi Mungu alimwekea na kuwatimizia waliosalia miongoni mwao sehemu zao. Na huku ni kulichagua jambo moja katika ya mambo bila sababu. Na kumpunguzia mmoja wao si muhimu zaidi kuliko mwingine. Basi hali ya pili ikawa ndiyo hali ya kipekee iliyo sawa. Nayo ni kwamba tunampa kila mmoja wao sehemu yake kadiri tuwezavyo, na tunashiriki baina yao, kama deni la wadai ambalo ni zaidi ya mali ya mdaiwa. Na hakuna njia ya kufikia hilo isipokuwa kwa 'Awl. Basi ikajulikana kwa hilo kwamba 'Awl katika urithi ilibainishwa na Mwenyezi Mungu katika Kitabu chake. Kinyume na njia hii yenyewe, majibu yanajulikana. Kwa maana, ikiwa watu wa mafungu maalum mafungu yao hayatamaliza mirathi yote, na kikabaki kitu ambacho hakina anayekistahiki kama vile 'Aaswib (yule ambaye huchukua chote kilichosalia) wa karibu wala wa mbali. Basi kuirudisha (mali iliyosalia) kwa mmoja wao kuliboresha hilo juu ya mengineyo bila ya sababu ya kulipa uzito. Na kumpa hiyo wengine miongoni mwa wale wasiokuwa jamaa wa karibu na maiti ni kwenda kombo, na kujipinda, na kuipinga kauli yake; "Na jamaa wa nasaba wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe zaidi katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu." Kwa hivyo, inabaki tu kwamba ni lazima irudishwe kwa watu wa mafungu maalum kulingana na mafungu yao. Na walipokuwa wanandoa wawili si katika jamaa wa karibu, hawakustahiki nyongeza juu ya mafungu yao waliyokadiriwa [kwa wale wanaosema kwamba hao hawaongezwi. Na ama kwa kauli sahihi kwamba hukumu ya wanandoa wawili ni kama hukumu ya warithi wengineo katika kongezwa, basi ushahidi uliotajwa hapo awali unawajumuisha wote kama ulivyowajumuisha ushahidi wa 'Awl (kuzidisha kiwango cha mirathi na kupunguza mafungu ya kila mrithi]. Na kwa hili pia unajulikana urithi wa jamaa wa maiti wasiokuwa na fungu maalum wala hawachukui kilichosalia. Kwani, ikiwa maiti hakuacha nyuma mrithi mwenye fungu maalum, wala mrithi anayechukua kilichosalia. Na suala hilo linabakia kuzunguka kati ya mali yake hiyo kwenda kwa hazina ya kitaifa kwa faida ya wasiokuwa jamaa za maiti, na kati ya mali yake kurudishwa kwa jamaa zake wanaotokana na warithi ambao imekubaliwa juu yao; basi hali ile ya pili inabakia kuwa ndiyo sahihi. Na hilo linaashiriwa na kauli yake Mtukufu, "Na ndugu wa tumbo wana haki zaidi wenyewe kwa wenyewe katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu." Basi kuipekela kwa wasiokuwa wao ni kumuacha yule anayestahiki zaidi kuliko wengineo. Kwa hivyo, ikabakia tu kuwarithisha jamaa wa maiti wasiokuwa na fungu maalumu wala hawachukui kulichosalia. Na kama itabakia tu kuwarithisha wao, ilikwisha julikana kwamba wao hawana fungu lililobainishwa kwa kila mmoja wao katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Na kwamba baina yao na maiti kuna waunganishi ambao kwa sababu yao waliingia katika jamaa, kwa hivyo wanateremshwa katika nafasi za yule anayewaunganisha katika hao waunganishi. Na Mwenyezi Mungu ndiye anayejua zaidi. Na ama urithi wa 'Aswaba waliosalia, kama vile wana wa kiume, na akina kaka na wana wao wa kiume, na akina ami na wana wao wa kiume n.k, basi Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - alisema, “Yaambatanisheni mafungu na wanaoyastahili, na chochote kinachobakia, basi ni cha 'asaba wa kiume." Na akasema Mtukufu, "Na kila mmoja tumemwekea warithi katika waliyoyaacha wazazi wawili na jamaa." Kwa hivyo tutakapoyaambatanisha mafungu na wanaoyastahiki, na hakuna kilichosalia, basi yule anayechukua kilichosalia atakuwa hastahiki kitu. Na ikiwa kuna kitu kilichosalia, anakichukua 'Aasib anayestahili zaidi kulingana na upande wake na daraja lake. Kwa maana, pande za wake wanaochukua mali iliyosalia ni tano: mwana, kisha baba, kisha kaka, kisha watoto wao wa kiume, kisha ami na watoto wao wa kiume, kisha mtumwa huru. Na anatangulizwa miongoni mwa yule wa upande wa karibu zaidi na maiti. Na ikiwa wako katika upande mmoja, basi anatangulizwa yule ambaye ndiye wa daraja la karibu zaidi. Na ikiwa wako katika daraja moja, basi anatangulizwa yule ambaye ni wa uhusiano wa nguvu zaidi, naye ni yule wa kwa baba na mama. Na ikiwa wako sawa kwa kila njia, basi watashirikiana. Na Mwenyezi Mungu ndiye anayejua zaidi. Na ama kwamba dada ambao si wa kwa mama wakiwa pamoja na mabinti au mabinti wa mwana wa kiume wanachukua kilichosalia mafungu yao, basi ni kwa sababu hakuna ushahidi katika Qur-ani kwamba dada wanaanguka kwa sababu ya kuwepo kwa mabinti. Kwa hivyo, ikiwa hali ni hii, na kitu kikabakia baada ya mabinti kuchukua mafungu yao, basi hicho watapewa madada. Na wala hawaachwi ili kuwapa 'Asaba wa mbali zaidi yao kama vile mwana wa kiume wa kaka, na ami, na yeyote aliye mbali zaidi nao. Na Mwenyezi Mungu ndiye anayejua zaidi.