Skip to content
Tafsir As-Saadi - Swahili · Az-Zumar
Sūrah 39

Az-Zumar

This is a translation of Tafsīr as-Saʿdī as IslamHouse.com publishes it at saadi.islamenc.com, read from that site’s pages. The site does not say who translated it or which printed edition it follows, and states no terms for taking its text, so the right to show it is not verified. Nobody has compared it with a printed book, and no scholar has reviewed it. Each passage stands beside the verses it comments on, which are the Qur’ān text of Tanzil, shown as it is there; a verse the site gives no commentary of its own stands with the passage before it, and the index names each such verse. Sabīl did not write or translate any of it.

Text fromsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)taken 2026-10-22

Verse 38

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ ٱلسَّمَـٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضَ لَيَقُولُنَّ ٱللَّهُ ۚ قُلْ أَفَرَءَيْتُم مَّا تَدْعُونَ مِن دُونِ ٱللَّهِ إِنْ أَرَادَنِىَ ٱللَّهُ بِضُرٍّ هَلْ هُنَّ كَـٰشِفَـٰتُ ضُرِّهِۦٓ أَوْ أَرَادَنِى بِرَحْمَةٍ هَلْ هُنَّ مُمْسِكَـٰتُ رَحْمَتِهِۦ ۚ قُلْ حَسْبِىَ ٱللَّهُ ۖ عَلَيْهِ يَتَوَكَّلُ ٱلْمُتَوَكِّلُونَ 38

{38} Yaani, ukiwauliza hawa wapotofu wanaokutisha kwa wasiokuwa Mwenyezi Mungu, na ukawathibitishia hoja kutokana nao wenyewe, ukasema: "Ni nani aliyeziumba mbingu na ardhi?" Hawataweza kuwathibitishia miungu wao hao chochote katika kuziumba, bali "bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu" peke yake ndiye aliyeziumba. "Sema" uwaambie kwa njia ya kuwafanya wakiri kutoweza kwa miungu yao baada ya kwisha bainishwa uwezo wa Mwenyezi Mungu: "Je, mnawaonaje wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa Mwenyezi Mungu akitaka kunidhuru" kwa ubaya wowote ule, "wao wanaweza kuniondolea dhara yake" yote kabisa au hata kuipunguza tu? "Au akitaka kunirehemu" kwa rehema ambayo kwayo atanifikishia manufaa katika dini yangu au dunia yangu, "je, wao wanaweza kuzuia rehema yake" isinifikie? Watasema: Hao hawawezi kuyaondoa madhara na wala hawawezi kuizuilia rehema yake. Basi waambie baada ya kwamba wameshabainikiwa na hoja ya kukata kwamba Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anayepasa kuabudiwa, na kwamba Yeye ndiye aliyeumba viumbe wote, Mwenye kunufaisha, kudhuru, na kwamba wasiokuwa Yeye hawawezi kwa namna yoyote ile kuumba wala kunufaisha wala kudhuru, ukiwaonyesha kwamba Yeye atakutosheleza na atakuzuia mbali na vitimbi vyao na njama zao. "Sema: Mwenyezi Mungu ananitosheleza. Kwake Yeye na wategemee wanaotegemea" katika kuwaletea manufaa na kuwakinga mbali na madhara. Kwani Yule mbaye pekee ndiye mwenye uwezo wa kutosheleza, Yeye ndiye atakayenitosheleza dhidi ya kila ninalolijali na nisilolijali.