Skip to content
Tafsir As-Saadi - Swahili · Al-Baqara
Sūrah 2

Al-Baqara

This is a translation of Tafsīr as-Saʿdī as IslamHouse.com publishes it at saadi.islamenc.com, read from that site’s pages. The site does not say who translated it or which printed edition it follows, and states no terms for taking its text, so the right to show it is not verified. Nobody has compared it with a printed book, and no scholar has reviewed it. Each passage stands beside the verses it comments on, which are the Qur’ān text of Tanzil, shown as it is there; a verse the site gives no commentary of its own stands with the passage before it, and the index names each such verse. Sabīl did not write or translate any of it.

Text fromsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)taken 2026-10-22

Verse 178

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ كُتِبَ عَلَيْكُمُ ٱلْقِصَاصُ فِى ٱلْقَتْلَى ۖ ٱلْحُرُّ بِٱلْحُرِّ وَٱلْعَبْدُ بِٱلْعَبْدِ وَٱلْأُنثَىٰ بِٱلْأُنثَىٰ ۚ فَمَنْ عُفِىَ لَهُۥ مِنْ أَخِيهِ شَىْءٌ فَٱتِّبَاعٌۢ بِٱلْمَعْرُوفِ وَأَدَآءٌ إِلَيْهِ بِإِحْسَـٰنٍ ۗ ذَٰلِكَ تَخْفِيفٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَرَحْمَةٌ ۗ فَمَنِ ٱعْتَدَىٰ بَعْدَ ذَٰلِكَ فَلَهُۥ عَذَابٌ أَلِيمٌ 178

{178} Mwenyezi Mungu Mtukufu anawakumbusha waja wake Waumini neema yake juu yao kwamba aliwafaradhishia “kisasi katika waliouawa.” Yani kufanya usawa katika hilo, na kwamba muuaji auawe kwa namna ambayo alimuulia aliyeuawa, ili kusimamisha uadilifu na haki kati ya waja. Na kuyaelekeza maneno haya kwa Waumini, kwa ujumla ndani yake kuna dalili kwamba ni wajibu kwao wote. Hata jamaa wa muuaji, hata muuaji mwenyewe, kumsaidia jamaa wa aliyeuawa; ikiwa ataitisha malipo na kuwezeshwa juu ya muuaji. Na kwamba hairuhusiki kwao kuzuia hadd hii (adhabu maalumu), na kumzuia jamaa huyo kufanya kisasi. Kama ilivyokuwa tabia ya Jahiliyya, na mwenye kufanana nao miongoni mwa wanaowapa wakosefu ulinzi. Kisha akabainisha undani wa hayo, akasema: “Muungwana kwa muungwana” anaingia katika tamko lake mwanamume kwa mwanamume, “na mwanamke kwa mwanamke” na mwanamke kwa mwanamume, na mwanamume kwa mwanamke. Na inakuwa kwamba, tamko lake lilitangulizwa mbele ya yanayofahamika katika kauli yake. “Mwanamke kwa mwanamke” pamoja na dalili ya Sunnah kwamba mwanamume huuawa kwa mwanamke. Na walitoka katika ujumla wa hili wazazi wawili hata kama watakwenda juu vipi. Hao hawauawi kwa mtoto wao, kwa sababu ya Sunnah inayoonyesha hilo. Pamoja na kwamba katika kauli yake “kulipiza kisasi,” kuna kinachoashiria kuwa siyo katika uadilifu kumuua baba kwa sababu ya kumuua mtoto wake. Na kwa sababu katika moyo wa baba wa huruma na rehema, kile kinachomzuia kumuua mtoto wake isipokuwa kwa sababu ya kasoro katika akili yake. Au madhara makubwa sana kutoka kwa mtoto wake. Pia ametoka katika ujumla huo ni kafiri kulingana na Sunnah, ingawa Aya inawazungumzia hasa Waumini. Pia, siyo katika haki kumuua rafiki ya Mwenyezi Mungu kwa sababu ya adui yake. Na mtumwa kwa mtumwa, awe mwanamume au mwanamke, thamani yao iwe sawa au tofauti. Na (aya) inaonyesha kwa maana yake isiyo ya moja kwa moja kwamba mtu huru hauawi kwa ajili ya mtumwa. Kwa sababu yeye (huru) sio sawa naye. Na katika “mwanamke kwa mwanamke,” na baadhi ya wanachuoni walizingatia maana yake isiyo ya moja kwa moja. Kwa hivyo hawakuruhusu kumuua mwanamume kwa ajili ya mwanamke, lakini kuruhusika kwa hilo kulikwisha tangulia. Na katika Aya hii, kuna dalili kwamba kanuni ya msingi ni ulazima wa kulipiza kisasi katika kuua. Na kwamba diya (fidia ya mauaji) ni badala yake. Ndiyo maana akasema: “Na anayesamehewa na ndugu yake chochote.” Yani jamaa ya aliyeuawa akamsamehe muuaji, na akakubali kuchukua diya (fidia ya mauaji) au baadhi ya jamaa wakasamehe. Basi hapo kisasi hakitakuwepo, na diya inakuwa lazima. Na hiari kati ya kisasi na kuchukua diya ni juu ya jamaa ya aliyeuawa. Ikiwa atamsamehe, basi itamlazimu jamaa [yani ya aliyeuawa] kumfuata muuaji [kwa wema] bila ya kumfanyia ugumu. Na wala kumbebesha kile asichoweza kustahimili. Bali afanye wema katika kudai na kuitisha, na wala asimfadhaishe. Na ni juu ya muuaji, “alipe kwa ihsani” bila ya kuchelewesha, wala kupunguza, wala kufanya ubaya kimatendo wala kimaneno. Je, malipo ya kumfanyia wema wa kumsamehe siyo isipokuwa (yeye) kufanya wema kwa kulipa vyema? Na haya yameamrishwa katika kila kilichothibitika dhima za watu miongoni mwa haki za wengine. Na ameamrishwa mwenye haki juu ya kuifuata kwa wema, ambaye haki iko juu yake kuilipa kwa wema. Na katika kauli yake,“ na anayesamehewa na ndugu yake chochote.” Kuna kufanya upole na kuhimiza kusamehe na kuchukua mali ya damu, na bora zaidi kuliko hilo ni kusamehe bure. Na katika kauli yake, “ndugu yake” kuna dalili ya kwamba muuaji hawi kafiri. Kwa sababu hapa kinachokusudiwa na udugu ni udugu wa imani. Basi hakutoka humo kwa kuua. Na katika mlango wa yale yanayofaa zaidi kuwa hivyo ni dhambi zinginezo zote zilizoko chini ya ukafiri; kwamba hawi kafiri kwazo mwenye kuzitenda. Bali hayo yanapunguza tu imani yake. Na ikiwa jamaa za aliyeuawa watasamehe, au baadhi yao wakasamehe, basi damu ya muuaji itahifadhika. Na atakuwa amehifadhika kutokana nao na kutokana na wengineo, na kwa ajili hiyo akasema: “Na atakayevuka mipaka baada ya haya.” Yani baada ya kusamehe, “basi yeye ana adhabu chungu,” yani katika Akhera. Na ama kuhusu kuua kwake na kutoua kwake, basi hayo yanachukuliwa kutoka kwa yale yaliyotangulia. Kwa sababu atakuwa amemuua aliye sawa naye, basi inalazima auawe kwa hilo. Ama yule aliyefasiri adhabu chungu kuwa ni kuua (muuaji baada ya kumsamehe), basi Aya hii inaashiria kuwa ni lazima auawe; na wala hairuhusiki kumsamehe. Na hilo ndilo walilosema baadhi ya wanachuoni, lakini lile la kwanza ndilo sahihi. Kwa sababu kosa lake la jinai halizidi kosa la jinai la wengine.