Al-Kahf
This is a translation of Tafsīr as-Saʿdī as IslamHouse.com publishes it at saadi.islamenc.com, read from that site’s pages. The site does not say who translated it or which printed edition it follows, and states no terms for taking its text, so the right to show it is not verified. Nobody has compared it with a printed book, and no scholar has reviewed it. Each passage stands beside the verses it comments on, which are the Qur’ān text of Tanzil, shown as it is there; a verse the site gives no commentary of its own stands with the passage before it, and the index names each such verse. Sabīl did not write or translate any of it.
Text fromsaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)taken 2026-10-22
قُل لَّوْ كَانَ ٱلْبَحْرُ مِدَادًا لِّكَلِمَـٰتِ رَبِّى لَنَفِدَ ٱلْبَحْرُ قَبْلَ أَن تَنفَدَ كَلِمَـٰتُ رَبِّى وَلَوْ جِئْنَا بِمِثْلِهِۦ مَدَدًا 109
{109} Yaani, waambie ukiwajulisha kuhusu ukuu wa Muumba na upana wa sifa zake na kwamba waja hawazunguki chochote kwazo, "Lau kuwa bahari" zinazopatikana katika ulimwengu "ingekuwa ndiyo wino kwa maneno ya Mola wangu Mlezi" na miti ya dunia hii tangu mwanzo wake hadi mwisho wake miongoni mwa miti ya nchi zote, na ya majangwani na ya baharini ndizo kalamu, "basi bahari ingelimalizika" na kalamu hizo zingevunjwa "kabla ya kumalizika maneno ya Mola wangu Mlezi." Na hili ni jambo kubwa ambalo hakuna yeyote anayeweza kulizunguka. Na katika aya nyingine, "Na lau kuwa miti yote iliyomo duniani ikawa ni kalamu, na bahari (ikawa wino), na ikaongezewa juu yake bahari nyingine saba, maneno ya Mwenyezi Mungu yasingelikwisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima." Hii ni njia ya kuleta maana karibu na akili. Kwa sababu vitu hivi vimeumbwa, na viumbe vyote vitatoweka na kuisha. Na ama maneno ya Mwenyezi Mungu, hayo ni katika sifa zake yeye Mtukufu, na sifa zake hazikuumbwa, wala hazina kikomo, wala mwisho. Basi upana wowote na ukuu wowote unaofikiriwa na mioyo, basi Mwenyezi Mungu yuko juu ya hivyo, na vivyo hivyo sifa zinginezo za Mwenyezi Mungu Mtukufu, kama vile elimu yake, hekima yake, uwezo wake, na rehema zake. Na ikiwa elimu ya viumbe ingekusanywa kutoka kwa wa mwanzo na wa mwisho, wakazi wa mbinguni na wakazi wa duniani, basi ingekuwa kwa kulinganisha na elimu ya Mkuu kidogo kuliko kama vile ndege mdogo anaposimama kwenye ukingo wa bahari, kisha akachukua kwa mdomo wake maji kutoka baharini humo kwa kulinganisha na bahari hiyo na ukuu wake, kwa sababu Mwenyezi Mungu ana sifa kuu, pana na kamili, na kwamba kwa Mola wako Mlezi ndio mwisho.